Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia mkataba wa ushirikiano na Ushirika wa Maisha Gemu wa Zanzibar kwa lengo la kusambaza nishati safi na salama visiwani humo.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo ilifanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala, alieleza kuwa mkataba huo utawezesha ushirika huo kusambaza kati ya tani 80 hadi 100 za nishati hiyo kila mwezi kwa kuanzia.
Magala alisema STAMICO imejipanga kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa nishati safi Zanzibar inatatuliwa kwa ufanisi, huku viwanda vitatu vya uzalishaji wa nishati hiyo tayari vikifanya kazi.
“Kwa sasa, tuna viwanda vitatu; Dar es Salaam, Kisarawe (Pwani), na Kiwira (Songwe). Aidha, tunajenga viwanda viwili zaidi Dodoma na Tabora. Tunafahamu changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati mbadala Zanzibar na Pemba, ambapo matumizi makubwa ya kuni na mkaa yanachangia uharibifu wa mazingira. STAMICO imejipanga kuondoa tatizo hili kwa kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa uhakika,” alisema Magala.
Magala aliongeza kuwa mkataba huo unaimarisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutunza mazingira.
“Niwashukuru Ushirika wa Maisha Gemu kwa kujitolea kuwa vinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi Zanzibar. Ushirikiano huu ni hatua kubwa kuelekea kufanikisha ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira,” alisema.
Pia alibainisha kuwa STAMICO imeongeza viwanda vya uzalishaji, huku mitambo mipya ikianza kazi Dodoma na Tabora, na kufanya jumla ya viwanda vikubwa vya uzalishaji kufikia vinne.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ushirika wa Maisha Gemu, Bw. Alawi Idarous, aliipongeza STAMICO kwa hatua hiyo na kuahidi kushirikiana kikamilifu kufanikisha utekelezaji wa mkataba huo.
“Tunashukuru STAMICO kwa kutufungulia fursa za kibiashara kupitia elimu ya Rafiki Briquettes visiwani Zanzibar. Tunahakikisha tunashiriki kikamilifu kutunza mazingira kwa kutumia nishati safi,” alisema Idarous.
Aliongeza kuwa matumizi ya Rafiki Briquettes yanatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa nishati safi Zanzibar na kusaidia juhudi za utunzaji wa mazingira.
STAMICO imeendelea kushirikiana na vikundi mbalimbali nchini kwa kuwapa nafasi ya kuwa mawakala na wasambazaji wa nishati safi. Ushirikiano huu unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.