Mohamed Kiganja- Katibu Mkuu Mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
Mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya, Bw. Emmanuel Kayuni (wapili kulia) akiwa na viongozi wa shirikisho hilo kabla ya kufungua mkutano mkuu uliofanyika jana Mkoani Mbeya.
Henry Kapera, Katibu Mkuu Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA)
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), wakisali kuwakumbuka wanamichezo wa shirikisho hilo waliofariki. Mkutano huo umefanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 12 hadi 13 Desemba, 2024
………………..
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Katibu Mkuu mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bw. Mohamed Kiganja amewataka wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali Tanzania na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha wanaisoma na kuielewa vema katiba ya Shirikisho hilo.
Bw. Kiganja ametoa kauli hiyo katika mkutano huo akiwa kama mgeni mwalikwa na kiongozi wa zamani wa Shirikisho hilo, ambapo imebainika kutokana na ugeni wa viongozi wa klabu hizo wanashindwa kuitafsiri vema sheria kwa mujibu wa katiba.
Bw. Kiganja amesema SHIMIWI inaongozwa madhumuni ambayo yanatengeneza mpango kazi wa kuufuata kwa shughuli zote za shirikisho.
Halikadhalika, Bw. Kiganja amesema vitu vingine vinavyosaidia kuendesha shirikisho ni kanuni ambazo zinatoa nafasi kulingana na maamuzi fulani ya mchezo fulani.
”Kitu pekee cha kuokoa mkanganyiko katika maamuzi fulani, basi ni kanuni kwa mfano timu mbili zimefungana kwa kila kitu wakiwa wamecheza mechi tatu na wamefungana kila kitu je mshindi anaweza kupatikanaje hapo, basi kamati inaweza kuamua wacheze uwanja huru, nayo hatua hii iwekwe kwenye kanuni“ amesema Bw. Kiganja.
Hatahivyo, amesema moja ya kazi za shirikisho ni kujenga viongozi wa baadae, ambapo kiongozi mzuri anaeleweka kutokana na matendo yake kwenye michezo.
Amesema sasa viongozi ambao wanakofia mbili za uongozi kwenye klabu yake pamoja na kwenye shirikisho, wanalazimika kuachia nafasi moja kwa mujibu wa sheria ya shirikisho hilo ya Bunge ya mwaka 1967 Iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1971 na marekebisho mengine ya mwaka 2018.
Amesema viongozi wa klabu wahakikishe wanakuwa na nidhamu kwenye michezo maana klabu hizo zina viongozi wa juu kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, na haitapendeza kuweka doa.
“SHIMIWI ni chombo kikubwa sana kuna mwenyekiti na viongozi wengine wa chini yake na hata wakifanya makosa wanajadiliwa kila mmoja binafsi, hivyo, viongozi wajitathmini na hata wanapokwenda kuchukua fomu za kugombea nafasi fulani wajione kama wanatosha kulingana na nidhamu zao,” amesema Bw. Kiganja.
Naye Katibu wa Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIISEMITA), Bw. Henry Kapera ameipongeza SHIMIWI kwa kuendesha shughuli kimkakati na kuwa shirikisho bora nchini.
Bw.Kapera ameliomba shirikisho hilo kuwajumuisha Afisa Utamaduni wa kila mkoa ili wawe kiunganishi cha ofisi za wakuu wa mikoa.