Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akilakiana na Mkurugenzi wa benki ya Dunia, anayesimamia Miundombinu, Bi. Wendy Hughes, alipofanya ziara ya kikazi nchini, ambapo Mkurugenzi huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri watatu wa Kisekta, akiwemo Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. Abdallah Ulega, ambapo walijadili kuhusu Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka-BRT, Ujenzi wa Mradi wa Treni ya Mwendo Kasi (SGR), na namna ya kuiwezesha sekta binafsi kwa kushirikiana na Sekta ya Umma kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha- Dar es Salaam)
……
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Benki ya Dunia imeshangazwa na hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali katika kutekeleza Mradi wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa wa SGR, na kuahidi kuwa itaweka mkono wake kusaidia ujenzi wa Reli hiyo muhimu kwa kukuza biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Benki ya Dunia anayesimamia Ujenzi wa Miundombinu, Bi. Wendy Hughes, aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri watatu wa Kisekta, wakiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. Abdallah Ulega.
Bi. Hughes aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete na Viongozi wengine waandamizi wa Benki hiyo, alisema kuwa amesafiri kwa kutumia reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kushangazwa na kiwango cha ubora wake wa viwango vya kimataifa.
Alisema kuwa Benki ya Dunia inaendelea kuchakata maombi yaliyowasilishwa na Serikali katika Benki hiyo, na kwamba iko tayari kusaidia ujenzi wa Reli hiyo ya Kimkakati na kushauri pia sekta binafsi ishirikishwe kikamilifu kuhakikisha kuwa malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa.
Wakizungumza katika kikao hicho kuhusu Mradi wa SGR, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mbarawa, waliishukuru Benki ya Dunia kwa kuamua kutoa fedha za kujenga mradi huo ambao umefikia hatua mbalimbali za ujenzi na ni mfano Barani Afrika na Duniani kwa ujumla
Walieleza kuwa Mradi wa SGR unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 10 za Tanzania, ni muhimu katika kuimarisha biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo si tu kwa Tanzania, bali katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo biashara kati ya nchi hizo inatarajiwa kuongezeka na kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa wananchi.
Mkutano huo uliowashirikisha Wakuu wa Taasisi katika Sekta ya Usafirishaji na Ujenzi, ulikuwa na ajenda tatu ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam-BRT, Mradi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa-SGR na namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza miradi kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPP.