Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Jumla ya Vitongoji 443, Vijiji 56, Mitaa 95 vinatarajia kunufaika kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 10, Disemba, 2024 katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo katika Kikao cha Kutambulisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Mkoani Ruvuma kwa Manispaa ya Songea na Songea Vijijini.
Aidha, Bw. Mbewa ametoa wito kwa jamii na watumishi kuupokea Mpango huo kwani una manufaa makubwa katika Sekta ya Afya.
“Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya Mikoa itakayokuwa ya Kipaumbele na Jumla ya Vitongoji 443 , vijiji 56 na mitaa 95 itanufaika kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na Jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 1076 watapatikana kupitia Mpango huo”amesema.
Halikadhalika, amesema Historia ya Wahudumu ya Afya katika Ngazi ya Jamii inaanzia mwaka 1970 ambapo walitekeleza Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kwa kuangazia masuala ya Elimu ya Afya , usafi wa Mazingira na kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza na Yasiyoambukiza.
Kwa Upande wake Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Bahati Mwailafu amesema katika zoezi la uchaguzi wa Wahudumu Ngazi ya Jamii itaitishwa Mikutano ya hadhara kuwe na uchaguzi wa huru na haki .
“Mikutano ya hadhara Ngazi ya vitongoji na mitaa itaitishwa ili Wananchi wachague mtu wanayemwamini na kutakuwa na Wahudumu wa Afya wawili kila Mtaa au kitongoji mwanamke na mwanaume”amesema.
Ikumbukwe kuwa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa tarehe 30, Januari, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ukiwa na Mikoa 10 ya kuanzia katika awamu ya kwanza .