Msemaji wa Simba Sports Club, Ahmed Ally, ametoa wito kwa mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mchezo muhimu unaotarajiwa kuchezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kundi la Kapu la Magoli, Ahmed Ally alisifu mchango wa kundi hilo katika kuhamasisha mashabiki wa Simba, hususan katika eneo la VIP B.
“Tumekuja kufanya uzinduzi kwenye Kundi la Kapu la Magoli kwa kutambua mchango wao ndani ya Simba Sports Club. Wamekuwa wakitengeneza hamasa kubwa kwa mashabiki wengine, na hii ni nguvu kubwa tunayoihitaji kuelekea mchezo wa Jumapili,” alisema Ahmed Ally.
Akihamasisha mashabiki wa Tandika na maeneo mengine, Ahmed Ally alisisitiza umuhimu wa kujaza uwanja na kuhakikisha kila Mwanasimba anakuwa sehemu ya mchezo huo muhimu.
“Watu wa Tandika, kwenda uwanjani kwenu ni karibu hata kwa mguu. Mnachotakiwa kufanya ni kununua tiketi tu. Hakuna Mwanasimba anayepaswa kubaki nyumbani siku hiyo. Tunahitaji kila mmoja ajitokeze na kuhakikisha tunaujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa,” aliongeza.
Pia, Ahmed Ally aliwakumbusha mashabiki kuwa jukumu la ushindi ni la kila Mwanasimba, si la wachezaji na viongozi peke yao.
“Wewe unayenunua tiketi ya Tsh. 3,000 usione ni jambo dogo. Unakuwa umeisaidia Simba kwa kiwango kikubwa. Ushindi unapatikana kwa nguvu zetu zote, kwa umoja wetu kama familia ya Simba,” alisema kwa msisitizo.
Licha ya mpinzani wao kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika michezo miwili ya awali, Ahmed Ally alionya dhidi ya kuudharau.
“Mpinzani wetu ni mwarabu, na muda wowote anaweza kuibuka. Jukumu letu ni kuhakikisha tunamzamisha kabisa na kuondoka na ushindi,” alihitimisha.
Mashabiki wa Simba wanatarajiwa kuonyesha mshikamano mkubwa na kuipa timu yao nguvu zaidi kuelekea mchezo huo wa kimataifa.