Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo akiongea na Washiriki wa mafunzo kuhusu nishati safi ya kupikia; mafunzo yalioendeshwa na REA kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) wilayani Bukombe, tarehe 10 Desemba, 2024.
Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo, akifunga mafunzo kuhusu nishati safi ya kupikia; mafunzo yalioendeshwa na REA kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA); (Kushoto) kwake ni Bwana Kelvin Nyema, Mtendaji Mkuu wa TAMAVITA na (Kulia) kwake ni Mhandisi, Kelvini Tarimo kutoka REA
Mwedesha mafunzo ya nishati safi ya kupikia kutoka REA; Mhandisi, Kelvini Tarimo akitoa mada kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia wilayani Bukombe.Washiriki wa mafunzo kuhusu nishati safi ya kupikia; wakimsikiliza Mhandisi, Kelvini Tarimo akitoa mada kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.Sehemu ya Washiriki kutoka katika makundi maalum ya wenye ulemavu wakifundishwa mambo mbali mbali kuhusu nishati safi ya kupikia.Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA); Bwana Kelvin Nyema ambaye ni kiziwi akitoa shukran baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya kuwajengea uelewa Watu wa makundi maalum kuhusu nishati safi ya kupikia kwenye warsha hiyo. Bi. Sailwa Balichene ambaye ni kiziwi akipokea jiko la gesi kutoka kwa Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu nishati safi ya kupikia, mafunzo yaliyotolewa na REA.Bwana Shaban Tangawizi ambaye ni kipofu akipokea jiko la gesi kutoka kwa Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu nishati safi ya kupikia, mafunzo yaliyotolewa na REA.
……………..
Wakala wa Nishati Vijijini (REA); tarehe 10 Desemba, 2024 imeendesha mafunzo maalum kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) na kisha kugawa majiko ya gesi ya kilo 6 kwa Watu wa makundi maalum wakiwemo Viziwi, Wasioona na wenye Ualbino wapatao 64 wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Akiongea katika hafla hiyo; Katibu Tawala wa wilaya ya Bukombe, Bwana Ally Mketo ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa Watu wa makundi maalum wakiwemo (Wasioona, Viziwi na wenye Ualbino) katika wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
“Ndugu zangu kama mnavyofaham nchi yetu sasa inatoka kutoka kwenye matumizi ya nishati za “kimila”; zisizo safi na salama kama kutumia kuni, kutumia mikaa na vinyesi vya ng’ombe kwa ajili ya nishati ya kupikia na sasa tunaelekea kwenye matumizi ya nishati safi na salama, nishati ambazo hazina athari kiafya na kwa mazingira”. Amesema Katibu Tawala wa wilaya, Ally Mketo.
Ameongeza kuwa siku za nyuma Wazee katika maeneo mengi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, walikuwa wanauwawa kwa kuhusishwa na imani za kishirikina kutoka na macho yao kuwa mekundu ambapo hali hiyo ilichangiwa na matumizi ya nishati zisizo safi na salama (Kuni na mkaa).
Bwana Mketo ametoa wito kwa Washiriki wa mafunzo hayo kuendelea kutumia nishati safi na salama ili kulinda afya zao pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa, yameribiwa kutokana na kukatwa hovyo kwa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Naye Mkufunzi, aliyeendesha mafunzo hayo kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Kelvini Tarimo amesema lengo la mafunzo hayo kuhamasisha na kuwajengea uelewa Wananchi kwa kuwa Serikali imekusudia kuwa makundi yote ya Watu kwenye jamii wanafikiwa kwa kuwa nishati ya kupikia inatumiwa na kila mtu.
“Lengo la Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watazania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, ili kufika huko tunaendelea kutoa elimu kwa makundi yote ya Watu ili wale wanapata mafunzo kama haya, wakaanze kutumia teknolojia za nishati safi ya kupikia na pia wakawe Mabalozi kwa wengine katika kuendeleza jitihada hizi za Serikali katika kuwaendeleza wengine katika matumizi ya nishati safi na salama.”Amesema, Mhandisi Kelvini Tarimo kutoka REA.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA); Bwana Kelvin Nyema, ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo hayo ya nishati safi ya kupikia na kisha kugawa majiko ya gesi kwa Watu wa makundi maalum (Viziwi, Vipofu na Wenye Ualbino).
“Mafunzo haya tuliyopata ni mazuri sana kwa kuwa yametuongezea uelewa kwa sisi viziwi, vipofu na walemavu wengine walioshiriki hapa; tunamshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kuwa tulimuomba kuhusu kupata mafunzo haya, na leo REA wamekuja na kutufundisha”
Pili, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ruzuku kwenye majiko ya gesi. Leo, Washiriki wa mafunzo haya, tumepata majiko 64”. Amesema, Bwana Nyema