Mwamvua Mwinyi, Pwani
Disemba 11, 2024
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kusirye Ukio, amebainisha kuwa matukio takriban 7,000 ya ukatili yaliripotiwa ndani ya mwaka mmoja mkoani humo.
Ukio alitoa taarifa hiyo wakati akizungumza kwenye kikao kilichowajumuisha viongozi wa mkoa, viongozi wa dini, watendaji wa halmashauri , ikiwa ni wiki ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuelekea Miaka 30 ya Beijing: Chagua Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia”,Kikao ambacho kilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Akiendelea kufafanua, Ukio alisema kati ya matukio hayo, asilimia 60 yanahusiana na ukatili wa kihisia, ikiwa ni pamoja na matumizi ya maneno yanayodhalilisha utu wa mtu.
Asilimia 30 ni ukatili wa kimwili, kama vile kupigwa au kuchomwa, huku asilimia 10 yakiwa ni matukio ya ukatili wa kingono.
Ukio alihimiza jamii kuhakikisha waathirika wa ukatili wanapata huduma za afya haraka ndani ya saa 72.
Alionya kuwa ,madhara makubwa, kama vile maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa, yanaweza kujitokeza endapo hatua za haraka hazitachukuliwa ndani ya saa 36.
Aidha, aliitaka sekta zote zinazoshughulika na kudhibiti ukatili wa kijinsia kushirikiana kuhakikisha matukio yanapunguzwa kwa kuchukua hatua za dharura na zinazofaa.
Akiangazia suala la kipindupindu, Ukio alisema Mkoa wa Pwani kwa sasa hauna mgonjwa yeyote wa ugonjwa huo, licha ya mikoa 23 kati ya 26 nchini Tanzania kuripoti maambukizi.
“Hatuna ripoti ya mgonjwa wa kipindupindu,Tushirikiane kwa kufuata ushauri wa kitaalamu ili kujikinga na ugonjwa huu,” alisisitiza Ukio, huku akiwapongeza wakurugenzi na wakuu wa wilaya kwa juhudi zao za kukabiliana na viashiria vya ugonjwa huo na kuzuia kuenea kwake.
Katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF Net) Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Batseba Kassanga, aliwaongoza maafisa, wakaguzi na askari kutoa msaada kwa akinamama katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kibaha, Mkaguzi wa Polisi Kijakazi Twalib, alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwajibika katika kuhakikisha watoto wanapata ulinzi dhidi ya ukatili.
Aliwataka wazazi kufuata miongozo inayosaidia kujenga watoto kiakili, kimwili, na kimaadili.