Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imewaasa waandishi wa Tamthilia nchini kushiriki katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ambayo inalenga kuwatambua na kuwazawadia waandishi bunifu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, amesema taasisi hiyo, kwa ushirikiano na Kamati Maalum ya Wataalamu, imekuwa ikihamasisha tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuzinduliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Kwa mujibu wa Dky. Komba, Tuzo ya Uandishi Bunifu imekuwa ikiongeza nyanja mbalimbali kila mwaka ili kuimarisha ushiriki wa wadau tofauti.
“Mwaka huu tumeongeza nyanja inayowahusu ninyi waandishi . Tunatamani muelewe umuhimu wa tuzo hii na kutumia nafasi hii kushiriki. Tuzo hii ina malengo mengi, lakini moja kuu ni kuongeza ushiriki wa waandishi wa Tamthilia na filamu. Hivyo, namkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, Prof. Penina Mlama, kuelezea zaidi kuhusu malengo ya tuzo hii,” alisema Dk. Komba.
Kwa upande wake, Prof. Mlama alisema kuwa lengo kubwa la tuzo hiyo ni kuwatambua na kuwazawadia waandishi bunifu waliobobea, ambao ni muhimu katika kuhifadhi na kurithisha utamaduni wa taifa.
“Waandishi bunifu wana mchango mkubwa sana katika historia ya taifa lolote. Aidha, tuzo hii inalenga kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, ambayo sasa imepata umaarufu ndani na nje ya Afrika,” alieleza Prof. Mlama.
Ikumbukwe kuwa Waziri Prof. Mkenda alizindua rasmi tuzo hiyo Novemba 17, 2024, wakati wa hafla ya uzinduzi wa vitabu vilivyoshinda tuzo hiyo kwa mwaka 2022-2023 na 2023-2024. Waziri alibainisha kuwa tuzo hiyo inalenga pia kuchochea Watanzania kuandika vitabu ili kukuza utamaduni wa usomaji nchini