Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Arusha katika kilele cha Siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia Mkoani humo wametoa mitaji kwa warahibu wa dawa za kulevya ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.
Akiongea wakati wa kukabidhi mitaji hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa huo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Georgina Matagi amebainisha kuwa baada ya serikali kutoa huduma ya tiba kwa warahibu hao, wameona ni vyema kuunga juhudi hizo kwa kutoa mitaji ya biashara ili iweze kuwaingizia kipato, kuwakwamua kiuchumi na pia kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha SSP Georgina ametaja baadhi ya misaada waliyoitoa kwa vikundi vya warahibu hao nivifaa vya saluni ya kike na kodi ya pango ya saluni hiyo kwa muda wa miezi sita ambapo jumla imegharimu Tshs 4,580,000/=, mtaji wa Tshs 500,000/= kwa ajili ya biashara ya matunda na mbogamboga, Tshs 500,000/= kwa ajili ya utengenezaji wa sabuni, na Tshs 500,000/= kwa ajili ya biashara ya mtumba.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Afya ya akili katika Hospitali hiyo yaRufaa Dkt. Salum Seifamesema kituo hicho kilianza na jumla ya warahibu 12 ambapo mpaka sasa kinahudumia warahibu 746 ambapo wameona ni vyema kupitia siku 16 za kupinga ukatili kuwashirikisha wadau ikiwemo Jeshi la Polisi ili kulifikia kundi hilo ambalo ni wahanga wa ukatili wakisaikolojia na uchumi.
Akimwakilisha mganga mfadhiwi wa hosipitali hiyo Bi. Angel Kimati amewapongeza warahibu wadawa za kulevya kwa uamuzi wao wa kufika katika kituo hicho na kupewa tiba huku akiwataka kutumia vyema mitaji waliyoipata Kwenda kukuza vipato vyao lakini pia kujikwamu kiuchumi na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia wakati wote.
Nae mnufaika wa Ratifa Abdi mbali na kulishukuru Jeshi la Polisi, amesema vitendea kazi na mitaji waliyopatiwa itawasaidia kuwaongezea vipato na Kwenda kuwa msaada mkubwa katika familia zao lakini pia kuwaepusha na matumizi ya dawa za kulevya.