…………………..
KATIKA kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini, jamii imeaswa kuacha vitendo vya ubaguzi kwa watoto wa kike na wanawake, na badala yake iwashike mkono maeneo ili waweze kutimiza ndoto walizonazo katika ujenzi wa Taifa.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa mafunzo ya ushonaji kwa jamii ya wasichana kutoka mazingira magumu Nyanzobe Makwaia, yaliyotolewa na Taasisi inayojihusisha na utunzaji wa mazingira ya Environment Conservation Community Of Tanzania(ECCT) kama sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia, Nyanzobe amesema kwa utafiti uliofanywa na taasisi mbalimbali, umebaini kwa asilimia kubwa waathirika wake ni wasichana na wanawake, hivyo kuna kila sababu kwa jamii kubadirika na kuchanana na mazoea.
” Watoto wa kike na wanawake ndiyo kundi kubwa linaloathirika na vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, utakuwa familia fulani ina uwezo wa kumsomesha mtoto wa kike ila haifanyi hivyo, lakini mtoto wa kiume anapelekwa shuleni” amesema
Amesisitiza kuwa hapo awali alidhani matukio hayo yalikuwa yakitendeka huko zamani lakini cha kushangaza hadi Sasa yapo licha ya kuwa elimu kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi hadi Sekondari inatolewa bure na Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kuhusu mafunzo hayo, Mratibu huyo amesema lengo lake ni kuwawezesha watoto hao wa kike kuwa na ujuzi ambao utawawezesha kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao jambo alisema pia litaweza kuwasaidia kuondokana na ukatili majumbani kwao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ‘ECCT’ inayoendesha mafunzo hayo Bi Lucky Michael, amesema mafunzo hayo yaliyoanza kwa kundi la wasichana 15 wanaotoka ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, ni sehemu ya kundi kubwa la wasichana wanaotarajia kuwapa mafunzo hayo.
Ameongeza wao kama ECCT pamoja na kuwapa elimu hiyo ya ujasiriamali, pia wanawafundisha namna ya kuepukana na matukio ya ukatili majumbani na hata katika jamii, wakiamini kuwa hiyo ni sehemu ya kuwajenga kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Amesema mbali na kuwapa elimu hiyo ya ujasiriamali, kupitia mafunzo hayo chini ya mradi ujulikanao kama ‘ECO WARE’ chini ya ufadhili wa Mfuko wa Women Fund Tanzania (WFT_T),yatawapa elimu wasichana hao juu ya utunzaji wa mazingira kupitia malighafi zinazotokana na mabaki ya vitambaa wakati wa ushonaji nguo.
Ends