Mh. Geophrey Pinda akizungumza katika mdahalo wa kumbukizi ya uhuru wa Tanganyika
…..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika, watanzania wametakiwa kuienzi amani tuliyonayo na kuepuka malumbano yasiyo na tija.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa ardhi mheshimiwa Geophrey Pinda wakati wa mdahalo wa miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara uliofanyika katika chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) ndaki ya Mizengo Pinda katika halmashauri ya Mpimbwe wenye kauli mbiu isemayo Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu.
Akizungumza katika mdahalo huo uliohusisha wakazi wa Mpimbwe, taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali, viongozi wa dini na siasa, wazee maarufu na wanafunzi wa SUA, mh. Pinda amewataka wananchi kuendelea kuiweka Tanzania katika hali ya amani na kufafanua kuwa vita si hali ya kujivunia.
“Hiki tulichonacho ni kwa sababu hakitoi sauti, sisi huku tunakaa kwa mchanganyiko mkubwa sana, hatuulizani wewe dini gani, wewe kabila gani, lakini kwa wenzetu huko hata maumbile tu yanawatofautisha!” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa tumshukuru Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutuunganisha na kuwa wamoja.
“Vita isikie kwa jirani si kwako” alisema.
Aidha, amegusia maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana ambapo alisema mwaka 2020 halmashauri ya Mpimbwe ilikuwa na vituo vya afya viwili na kufikia sasa kuna vituo vya afya saba na hospitali moja ya wilaya, shule za sekondari zilikuwa nne na sasa zipo 13 huku shuke nyingine mbili zikiendelea kujengwa.
Kwa upande wa shule za msingi zilikuwepo shule 21 na mpaka sasa zimeongezeka na kuwa na idadi ya shule za 54.
Kuhusu ardhi amesema serikali inaendelea na mpango wa matumizi bora ya ardhi na hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuitunza ardhi waliyonayo kwani ardhi haijawahi kuongezeka bali binadamu ndio wanaongezeka kila kukicha.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga amesema katika kuadhimisha miaka 63 wamefanya matukio mbalimbali ikiwemo kupanda miti katika maeneo ya vyanzo vya maji, na kufanya usafi katika maeneo ya umma kama masoko, stendi ya mabasi na hospitali.
Alisema kushirikiana na asasi za kiraia kama UDESSO wamepanda miti zaidi ya 1,000 katika eneo la hifadhi ya WMA na asasi ya WASIMA wamepanda miti zaidi ya 1,500 katika eneo la mlima wa Wamweru.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe bi. Shamimu Mwariko amewataka vijana kuenzi mila na desturi tulizonazo kwani zina sifa na uzuri tulionao Watanzania.
Bi. Mwariko pia amewataka vijana kuwatunza wazee kwani wazee ni tunu ya Taaifa na kuacha kuiga mambo ya kigeni.
Katika mdahalo huo watu mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia mada ya tulipotoka na namna tulivyo sasa ambapo mzee Alexandra Maperani mwenye umri wa miaka 77 alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.
Mzee Maperani alisema zamani walitegemea zaidi mitishamba katika matibabu kutokana na hospitali kuwa chache lakini sasa huduma za matibabu zimesogezwa karibu na wananchi.
Watu wengine walioshiriki mdahalo huo waliishukuru serikali kwa kuendelea kuhimiza upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi ikiwemo maji, elimu, afya, nishati ya umeme na barabara.
Halikadhalika wameahidi kushirikiana na serikali katika kutunza amani ya nchi yetu.