NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na kubadilishana mawazo wakati akimfariji Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Bi.Mwaka Mrisho Abdalla (wa kwanza kushoto) katika ziara yake ya kumtembelea kiongozi huyo anayesumbuliwa na matatizo ya kiafya, katika ziara hiyo amepokelewa na Katibu wa Mkoa huo Abdalla Mwinyi Hassan (wa pili kulia).
……………
Na Is-haka Omar,Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amemtembelea na kumjulia hali yake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Bi. Mwaka Mrisho Abdalla, anayeumwa kwa muda mrefu.
Dkt. Dimwa, alikwenda nyumbani kwake kijijini Ubago Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja kwa lengo la kumfariji na kumtakia afya njema, sambamba na kumwombea apone haraka na kurudi katika shughuli za uongozi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa alisisitiza umuhimu wa kuwa na utamaduni wa kutembeleana na kubadilishana mawazo miongoni mwa wanachama, viongozi, na makada wa chama.
Alieleza kuwa utamaduni huu unaleta umoja, mshikamano, na upendo miongoni mwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.
Aliongeza na kusema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha mwanachama yeyote anayepata changamoto za kiafya kufarijiwa ili apate faraja ya kuwa wanachama na viongozi wanamjali na kumthamini.
Dkt. Dimwa alikumbusha kwamba CCM Zanzibar itaendeleza utaratibu huo wa kutembeleana na kujali hali za viongozi na wanachama wake kwa lengo la kuenzi na kudumisha misingi ya umoja na mshikamano iliyojengwa na waasisi wa Chama Cha ASP, chini ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume.
Aidha, alisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuendeleza miradi ya maendeleo ambayo inafaida kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar, akieleza kwamba CCM itaendelea kudumisha na kutekeleza mafanikio yote yaliyopatikana katika sekta mbalimbali, ambayo ni matunda ya juhudi na maono ya waasisi wa chama.
Dkt. Dimwa alitoa wito kwa wanachama, viongozi, na watendaji wa chama kuendelea kuwa na mshikamano na kushirikiana katika kazi za maendeleo, ili kuimarisha na kuendeleza ustawi wa Zanzibar, kama ilivyokusudiwa na waasisi wa taifa hili.
Aidha, Dkt. Dimwa alikumbusha kuwa CCM itaendelea kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kutatua changamoto za wananchi, hususani katika sekta za afya, elimu, miundombinu, na uchumi.
Alisema kuwa maendeleo haya ni matokeo ya juhudi za serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bazara la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi pamoja na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,na kwamba CCM itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.