NA DENIS MLOWE. MAFINGA
WITO umetolewa kwa vijana wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kuwa wazalendo wa kweli na kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa leo kata ya Mdabulo kwenye tamasha la kizalendo na mdau wa maendeleo wilayani humo, Shalom Robert alipokuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la michezo mbalimbali .
Shalom ambaye kitaaluma ni mwanahabari alitoa wito huo kwa mamia ya vijana waliohudhuria tamasha hilo alisema uzalendo si gharama kubwa bali ni kujitoa kwa dhati kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Ndugu zangu, kuwa wazalendo katika nchi yetu si gharama kubwa ni moyo wa kujitoa na kuwa na imani kubwa kwa viongozi wetu wa nchi Lakini pia ni lazima mzitambue na kuzitumia kwa vitendo fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yenu ili muwe msaada mkubwa kwa jamii,” alisisitiza.
Aidha, Shalom aliwakumbusha vijana kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kuleta maendeleo na kuhakikisha wanakuwa nguzo ya mabadiliko ya kijamii. Aliongeza kuwa kwa kutambua na kutumia rasilimali zilizopo ndani ya wilaya yao, vijana wanaweza kufanikisha mambo makubwa, ikiwa ni pamoja na kujenga uchumi imara wa mtu binafsi na jamii nzima.
Pia alitoa shukrani kwa vijana kwa kuiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, na kuwapongeza kwa kuonyesha mshikamano wa kisiasa na kiutendaji.
“Ninawapongeza kwa uamuzi wenu wa busara wa kuchagua viongozi wa CCM katika uchaguzi uliopita.
Kuwa huu ni uthibitisho wa imani yenu kwa chama kinachoendelea kuwaletea maendeleo,” alisema Shalom.
Tamasha hilo la michezo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, akiwemo Diwani wa Kata ya Mdabulo, Ernei Nyeho.
Viongozi hao walisisitiza mshikamano na umuhimu wa michezo kama njia ya kuimarisha afya, kujenga urafiki, na kuleta maendeleo ya kijamii.
“Tunapenda kuona vijana wakijituma, wakijifunza, na kutumia fursa zilizopo. Mtakapokuwa na bidii, uzalendo, na mshikamano, mtakuwa msingi wa taifa imara na lenye maendeleo,”