*Asema waliohusika na tukio hilo lazima wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
*Asisitiza ifike wakati Dola lazima iheshimike.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amelaani vikali kitendo cha kushambuliwa kwa watumishi wa TRA wakati wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria eneo la Tegeta Wilaya ya Kinondoni na kupelekea kifo cha Ndg Amani Kamguna Simbayao ambaye alikuwa Dereva wa Gari hilo.
RC Chalamila ametoa pole kwa Ndugu jamaa na marafiki kufuatia msiba huo ambapo amesema waliohusika na tukio hilo lazima wakamatwe wote ili sheria ichukue mkondo wake ” Lazima ifike wakati Dola iheshimike” Alisema Chalamila.
Vilevile RC Chalamila alipendekeza namna bora ya kumuenzi marehemu kupitia kuisaidia familia yake ikiwemo mama na watoto kwa kuanzisha mfuko maalum (Bound) ambao utachangiwa na watumishi wa TRA na Wizara ya Fedha na wadau wengine, baadaye fedha hizo zitumike kwa ajili ya kuwasomesha watoto wa marehemu.
Aidha tukio la kuaga mwili wa Amani Simbayao limefanyika katika viwanja vya TRA kurasini na kuongozwa Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba ambaye amesema kitendo kilichofanyika hakivumiliki ameagiza Mkuu wa Mkoa na kamati zake za usalama wahakikishe waliohusika wote wanakamatwa mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa Kamishna Mkuu wa TRA Ndg Yusuph Mwenda amesema watumishi hao walikuwa wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria hivyo shambulio lilowakuta ni kinyume cha sheria ambapo amesisitiza TRA itaendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi waelewe majukumu ya taasisi hiyo muhimu kwa masilahi mapana ya mwananchi mmojammoja na Taifa kwa Ujumla hivyo kila mmoja anapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwa TRA