Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Vijijini Kwangwala Misana wakati akipanda mti katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania Bara katika shule ya Sekondari ya wasichana Rukwa
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga wakiadhimisha siku ya uhuru kwa kufanya usafi katika soko la Laela
Mhifadhi Mwandamizi Wakala wa msiti TFS wakati akipanda mti katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Rukwa katika mji wa Laela
Na Neema Mtuka
Sumbawanga, Rukwa
Katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara ,Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imetoa miche ya miti 1000 kwa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Rukwa iliyopo katika Mji wa Laela ili kuweza kuboresha na kutunza mazingira.
Miti hiyo imetolewa katika shamba la miti la Mbizi Forest linalosimamiwa na wakala huo ambayo imepandwa na wanafunzi na watumishi wa umma kwenye maeneo ya shule hiyo.
Maadhimisho ya siku hii ya uhuru hufanyika kila mwaka tarehe 9 Disemba ambayo kwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 63 tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania Bara ukiwa na kauli mbiu isemayo “Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu”
Katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan alitangaza kufuta sherehe ,na badala yake fedha zilizopangwa kufanya shughuli hiyo zimeelekezwa kwa jamii.
Akizungumza na wananchi wa Laela leo Dec 9 2024 Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga Gabriel Masinga amewataka wananchi kuendelea kupanda miti na kutunza sambamba na kutunza afya zao kwa kufanya mazoezi ya mwili.
Pia amewataka kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuilinda amani na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa umoja na utulivu kama nguzo ya mafanikio.
“Hakuna uhuru wa taifa kama hakuna uhuru binafsi hatuwezi kuulinda uhuru wa taifa kama hatuwezi kuulinda uhuru binafsi tujikomboe kifikra kiuchumi tunaweza kuikomboa nchi kama taifa na kuhakikisha kwamba tunaulinda uhuru wetu”
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika tukio hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga vijijini Kwangwalu Misana amesema wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa laela na kushiriki zoezi la kupanda miti katika shule ya Sekondari ya wasichana ya mama Samia ya Laela.
“Miche hii ya miti tuliyoipanda ni kielelezo tosha cha kuwa tunataka mazingira yaendelee kutunzwa kwa kuhakikisha kila mwanafunzi katika shule hii analinda mche wake jambo hilo litasaidia kuitunza.”alifafanua
Nao baadhi ya wanafunzi na wananchi akiwemo Didasi Nzowa na Ananilea Wloson wamesema watailinda miti hiyo kwa kuimwagilia na kuhakikisha inawekwa mbolea ili iweze kukua vyema .
Mhifadhi Mwandamizi wa wakala wa misitu Tanzania Adolf Peter Mara amewataka wanafunzi na wananchi hao kuitunza miche hiyo ya miti na kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuachana na kasumba ya kupanda miti na kuitelekeza .
“Itunzeni miche hii ya miti nayo itawatunza kwa kupata hewa safi kivuli na matunda ambayo yataboresha afya zenu”.
Halmashauri ya wilaya ya sumbawanga iliyopo mkoani Rukwa imeadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara kwa kufanya usafi katika soko la Laela ,kutembelea wagonjwa na kupanda miti 1000 katika shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Rukwa katika mji wa laela.