SOPHIA KINGIMALI.
WATANZANIA Bara na Visiwani wametakiwa kutumia fursa ya elimu inayotolewa bure katika Chuo cha Veta Furahika ili kujitapatia ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kimaisha
Lakini pia wanafunzi wanaohitimu kwenye chuo hicho wametakiwa kuwa mfano wa kuingwa kwa jamii kwa kufanya kazi kwa weredi na kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Hayo yamesemwa na katibu wa Jumuia ya wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Janus Mfaume akimwakilisha Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, Abbas Mtevu katika mahafali ya Chuo cha VETA Furahika ambapo wahitimu 415 wamehitimu katika kozi mbalimbali wakiwemo wahitimu 120 wanaotoka Zanzibar.
Amesema kwamba katika Jumuia hiyo wana kanuni inawaelekeza kuwa kama mawakili wa jamii kwa kuchagiza na kutoa msukumo kwa watu kuwekeza kwenye taaluma na kuandaa kizazi chenye mwelekeo wa kuhudumia jamii.
“Kwetu hii ni fursa kubwa na mmeona Mkuu wa Chuo ameeleza kwamba asilimia 80 ya wanaosoma hapa wamepatikana kupitia ushawishi wa Jumuia ya Wazazi CCM, kuanzia katika Matawi hadi Kata kwa kuleta watoto ambao wameonekana kukata tamaa na wanafanikiwa kujiendeleza kielimu na kuinua ndoto zao.
“Hivyo nitoe wito kwa wazazi wa Tanzania Bara na Visiwani kuleta vijana wao ambao wamekwama kuendelea na elimu na hapa watapata elimu bure kwa kujifunza kozi wanazotaka kama vile umeme, Compyuta, hotelia, bandari na nyinginezo zitakazowasaidia kujiajiri ama kuajiriwa,” amasema.
Sambamba na hayo amepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa ufadhili kwa vijana hususan wa kike, kusoma katika chuo hicho ili kutimiza ndoto zao ambao zilionekana kupotea kutokana na changamoto mbalimbali ambazo wamepitia.
Aidha amewataka wahitimu hao kuzingatia maadili katika majukumu yao ya kazi ili wawe mabalozi wazuri wa Chuo hicho ili vijana wengine wavutike kwenda kuchukua ujuzi utakaowafaa katika maisha yao.
Naye Sitti Abbas Ally, ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Zanzibar, amesema wasichana 120 ambao wamehitimu wametoka katika mikoa mitano na wilaya 11 visiwani humo na kutanabaisha kuwa kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa ndio maana imetoa sh. mil 100 kwa ajili ya wasichana hao kusoma katika chuo hicho.
“Pia nawaomba wahitimu kwamba wasiangalie ajira za Serikali pekee au za kuajiriwa kupitia ujuzi ambao wamepata wanaweza kuajiriwa na kuajiri wengine na Januari 2025 tutatoa wanafunzi wengine 300 kuja chuo cha Furahika kwa ajili ya masomo.
“Tunaishukuru Serikali ya Zanzibar kwa kutoa mil. 100 kwa ajili ya wanafunzi hawa ambao wamehitimu leo na wakati tunaomba fedha hizo walitoa bila kinyongo tena kwa mapenzi makubwa kwa kundi hili”, amesema.
Naye,Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt David Msuya amesema kuwa katika mafahali hayo wanafunzi 415 wamehitimu masomom katika fani mbalimbali ikiwemo urembo, upambaji, ushonaji, hotelia, umeme, bandari na nyinginezo.
“Ninafuraha kubwa kuona wanafunzi ambao wamefadhiliwa na Serikali ya Zanzibar, wakiwa wamehitimu vizuri na ninamshukuru Rais wa Dkt. Mwinyi kwa moyo wake wa upendo kwa vijana hawa kwani kama angewaacha, pengine wangeshindwa kutimiza ndoto zao, kikubwa tumuombee Mungu aendelee kuwa na afya njema na kusaidia wengine na tuko tayari kuwapokea,” amesema.