*Asisitiza kuongeza ubunifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma
*Awataka kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa maadili
*Wizara ya Nishati yaipongeza REA kwa utekelezaji wa miradi
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, ubunifu, juhudi, maarifa na upendo ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Dkt. Khatibu Kazungu wakati akifungua Baraza la Tano la Wafanyakazi wa REA leo tarehe 7 Disemba, 2024 katika ukumbi wa Ledger Plaza, Bahari Beach Hotel jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kazungu amewataka watumishi REA kuwahudumia Watanzania kwa maarifa na upendo hususan katika kufikia malengo ya Serikali yanayotarajiwa katika Sekta ya Nishati.
“Niwasisitize wajumbe wa mkutano huu kusikiliza kwa umakini, kufuatilia na kutoa maoni na ushauri utakaokuwa chachu ya kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora ya nishati kwa wananchi,” amesisitiza Dkt. Kazungu.
Aidha, amewaagiza watumishi REA kufanya kazi kwa ubunifu huku wakizingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Vile vile, amewataka kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa maadili kama vile rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kazungu ameipongeza REA kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati na kuwaahidi kuendelea kutoa ushirikiano na kuwaunga mkono kwa manufaa ya umma.
Naye, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Bw. Heri Mkunda ameipongeza Menejimenti ya REA kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyakazi na kusisitiza na kuomba ushirikiano huo uimarishwe ili kuongeza ufanisi na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Awali Mkurugezi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy ameeleza kuwa uhusiano wa Menejimenti na Wafanyakazi umeimarishwa katika nyanja zote na kuahidi kuendelea kuahirikiana na TUGHE ili kuongeza ufanisi wa wafanyakazi katika utendaji kazi.