Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania [TPA] inakusudia kukiimarisha Chuo cha Bandari Dar es Salaam ili kiweze kukidhi mahitaji ya Utaalamu wa utoaji huduma za kibandari katika Nchi za Afrika Mashariki.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara katika Mahafali ya 23 ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam yaliyofanyika Desema 06 2924 katika Viwanja vya Chuo hicho.
Prof. Kahyarara amesema, Serikali inachukua hatua za makusudi za kuimarisha Sekta ndogo ya Bandari Nchini kwa kuboresha Bandari zake kwa kuzioatia miundombinu ya kisasa, mitambo na teknolojia mpya pamoja na kukiimarisha Chuo hicho ili kutoa Wataalamu wenye Weledi na Umahiri unaohitajika katika soko la huduma za kibandari Nchini na Duniani.
Prof Kahyarara ameongeza kuwa, baada ya uamuzi wa Serikali kushirikiana na Sekta binafsi katika kuendesha na kuendeleza Sekta ya Bandari Nchini, kumekuwa na mahitaji ya kuboresha Sheria ya Bandari na Mafunzo ya Chuo cha Bandari ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ukuaji huo ambapo Serikali imeanza utekelezaji wake.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Juma Kijavara amesema, uimarishaji wa Chuo cha Bandari ni hitaji la lazima linalotekelezwa hivi sasa na Mamlaka ili kwenda sambamba na Mikakati iliyowekwa ya kuongeza idadi ya Meli na kiwango cha Shehena kinachohudumiwa ili kuongeza mchango wa Sekta ya Bandari katika Pato la Taifa na ukuaji wa Sekta nyingine Nchini.
‘ Tutaongeza miundombinu ya Majengo, Vifaa vya kisasa vya kutolea Mafunzo na mazingira mazuri kwa Watumishi wa Chuo hiki ili kuhakikisha kuwa, Wahitimu weti wanapata Weledi na sifa stahiki za kuhimili ushindani katika Soko la ajira na ufanisi katika sehemu za kazi, iwe Bandarini, katika Bandari Kavu au sehemu nyingine..
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Bandari Dkt. Lufunyo Hussein amesema, Chuo hicho kimejikita katika kufanya utafiti unaotoa suluhisho la mahitaji ya ujuzi, weledi na umahiri katika kuhudumia Meli na Shehena na kuwaalika Wadau wote wa Sekta ya Bandari kukitumia Chuo hicho.
Dkt. Lufunyo ameongeza kuwa, ushirikiano wa Chuo hicho na Taasisi mbalimbali za Kimataifa umeanza kuzaa matunda kwa kuanisha maeneo ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kuwajengea uwezo Wakufunzi wa Chuo katika Taasisi hizo nje ya Nchi.
Jumla ya Wahitimu 794 wamehitimu Mafunzo yao katika ngazi za Astashahada na Stashahada za uongozaji Meli, upokeaji na uondoshaji wa Shehena na shughuli za usafirishaji Majini.