…………………
Na Mwandishi wetu -Dodoma
Jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Utalii imeendelea kuungwa mkono na wadau mbalimbali hususani wanataaluma wa vyuo vikuu nchini ili kuhakikisha adhama ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuongeza idadi ya watalii inafanikiwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) Dkt. Betty Amosi Begashe, katika utafiti wa Shahada yake ya Uzamivu alisukumwa kuangazia “Sifa za kijamii na motisha za kusafiri: Chaguo la mwelekeo wa vivutio kati ya watalii wa kimataifa wa kurudia nchini Tanzania” ili kupata majibu ya changamoto ya watalii wengi kuto kurudi tena nchini kutalii na nini kifanyike kutatua changamoto hiyo.
Akiwa Jijini Dodoma baada ya kutunukiwa Shahada yake hiyo ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Begashe amesema kuwa Tanzania inasifika kwa vivutio vya aina mbalimbali lakini idadi ya watalii wanaorudia bado ni ndogo ikilinganishwa na baadhi ya nchi za Afrika ambazo ni washindani wake.
“Hii inaweza kuwa kutokana na ukweli kwamba, maswali kuhusu ni akina nani hasa hawa watalii wanaorudiarudia kwa mujibu wa sifa zao za kijamii, na watalii hawa wanakwenda wapi na kwa nini wanachagua mwelekeo fulani wa kivutio juu ya wengine haujulikani”. Alisema Dkt. Begashe
Dkt. Begashe ameongeza kuwa utafiti huo unanuia kubainisha mifumo ya vivutio na kuchunguza jinsi sifa za kijamii na na motisha za usafiri zinavyoathiri uchaguzi wa vivutio vilivyotambuliwa.
“Kwa hivyo wauzaji wanaweza kugawa soko hili na watoa huduma za utalii wanaweza kuunda vifurushi maalum vya watalii ili kuhakikisha watalii wanaridhika hali itakayo wavutia kurudi tena nchini” Aliongeza Dkt. Begashe
Aidha Dkt. Begashe licha ya kushauri wahusika katika sekta ya Utalii kutumia tafiti hiyo ili isaidie kuiwezesha Sekta ya Utalii iweze kuingiza mapato makubwa zaidi ya sasa kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake.