Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kwanza cha Mashauriano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE mjini Abu Dhabi tarehe 05 Desemba 2024.
Kupitia mazungumzo hayo ya kwanza na ya aina yake, Tanzania na UAE zimehakikishiana dhamira zao za kuendelea kushirikiana kwa karibu kuboresha uhusiano uliopo ili kuufikisha katika viwango vya juu kwa manufaa ya nchi na wananchi wa pande zote mbili.
Aidha, Tanzania na UAE zimeongelea pia umuhimu wa kushirikiana kiuchumi na kuwa na ushirikiano wa kina uliojengwa juu ya msingi wa kuaminiana, ambao umeyafanya mataifa haya kushirikiana kwa karibu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya pande mbili na ya kimataifa kwa maslahi ya pamoja
Pamoja na mambo mengine kupitia mashauriano hayo Tanzania na UAE zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara , uwekezaji, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hususan kwenye mpango wa Tanzania wa Build Better Tomorrow (BBT), Ujenzi na Usafirshaji, Nishati; Afya na Uchumi wa Buluu.
Aidha, kwa upande wa Nishati UAE imekubali ombi la Tanzania la kuunga mkono Agenda ya Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking Initiative) inayopewa msisitizo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuungwa mkono na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Dunia kwa ujumla kwa kuwa sio tu unamkomboa Mwanamke lakini pia inachangia katika agenda ya Dunia ya utunzaji wa mazingira.
Katika kutekeleza makubaliano tajwa pande zote mbili zimekubaliana kukamilisha na kusaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano hususan ya ya kiuchumi kwa maslahi ya wote.
Sambamba na hilo, Tanzania na UAE zimekubaliana kuharakisha utekelezaji wa mradi wa Upanuzi na Ukarabati wa Hospitali ya Wete, Pemba ambayo inatekelezwa kwa ufadhali wa Mfuko wa Maendeleo ya Abu Dhabi kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 10 pamoja na utekelezaji wa Mkataba kati ya Mfuko wa Maendeleo wa Khalifa (Khalifa Fund) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Msaada wa Dola za Marekani Milioni 10 kwa ajili ya Miradi ya Wajasiliamali Wadogo na Wakati Zanzibar.
Akizungumza katika majadiliano hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya siasa wa UAE Mhe. Lana Nusseibeh alisema Tanzania ni moja ya wadau wakubwa wa UAE barani Afrika na kuongeza kuwa hali hiyo imesababisha kusainiwa kwa Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya Anga na Kutotoza Kodi Mara Mbili .
Kupitia mikataba hiyo Mashirika ya Ndege ya Emirates, Etihad na FlyDubai pamoja na Air Tanzania yamepata kibali cha safari za moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili.
Kikao hicho cha kwanza cha mashauriano ya kidiplomasia kimekuwa cha mafanikio na kimefanyika wakati ambapo Tanzania na UAE zinaadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia na sasa umejikita katika ushirikiano wa kiuchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.