Naibu Katibu mkuu Wizara ya Elimu, Prof Daniel Mushi, akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)
Mkuu wa Chuo cha Ufundi,Arusha,Profesa Mussa Chacha, akizungumza kwenye mahafali hayo mkoani.Arusha
……….
Happy Lazaro, Arusha
WAHITIMU katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) wametakiwa kuitumia kwa ufanisi elimu waliyoipata, sambamba na kuwa waadilifu, wazalendo, wachapa kazi na kuheshimu dhamana watakayopewa kwani ni wajibu wao kutumia taaluma zao kutoa huduma kwa jamii kwa bidii na haki.
Aidha wametakiwa kuwa makini katika utendaji na utumiaji wa ujuzi na taaluma zao ambapo huku wakitumia mahafali hayo kuwa changamoto kwao wahitimu pamoja na wanafunzi wanaondelea na mafunzo katika kutumia taaluma zao kutatua changamoto zinazowakabili wao wenyewe, wananchi na Taifa kwa ujumla,changamoto hizo mzigeuze kuwa fursa ya ajira na maendeleo.
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Elimu, Prof Daniel Mushi,kwenye mahafali ya 16 ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo wanachuo, 1,139 wakiwemo wanaume 886 na wanawake 253 wamehitimu kozi katika ngazi mbalimbali zikiwemo Stashahada, Astashahada na Shahada .
“NIngependa kuwapongeza Wahitimu wote ambao leo hii mnatunukiwa vyeti vya kuhitimu. Ninategemea kuwa nyie Wahitimu wa Ufundi stadi (Artisans), ufundi Sanifu (Technicians) na Uhandisi (Engineers), bila shaka mnatambua hazina kubwa ya Elimu mliyoipata.”amesema.
Amesema kuwa Wizara inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hicho katika kutoa wataalamu ,kama Wizara inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya Ujenzi wa majengo yake kwa kutumia wataalamu kutoka chuoni hapo kutokana utaalamu wao mkubwa na Wizara imeboresha mitaala ili kuwezesha wahitimu kwenda kwenye Soko la ajira.
Prof Mushi,amesema kuwa Mahafali hayo yawe ni chachu na fursa ya ajira na maendeleo na dunia inakoelekea ni kujijenga zaidi kwenye ujuzi na Ufundi hivyo ni wajibu wao wahitimu hao kutumia taaluma zao kuihudumia Jamii na nchi yetu haiwezi kubakia nyuma katika matumizi ya teknolojia hivyo Ufundi unahitaka sana katika maendeleo ya uchumi nchi.
Awali Mkuu wa Chuo cha Ufundi,Arusha,Profesa Mussa Chacha,amesema Chuo hicho ,kimejenga tawi jipya Kijiji cha Kikuletwa Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuwaandaa Vijana wa nchi za Afrika mashariki kwa mafunzo ya Nishati Jadidifu .
Ameongeza kuwa,chuo kinakamilisha Ujenzi wa Hospitali iliyopo ndani ya eneo la Chuo hicho ambayo itaanza kutoa huduma ya matibabu kwa wanachuo na Wananchi mwezi Machi mwakani.
Amesema kuwa Chuo hicho kimetekeleza maelekezo ya Rais ya kutengeneza mita za Maji za malipo kabla ili kuondoa malalamiko ya wateja wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Jijini Arusha,AUWSA ya kubambikiwa Ankara.
Profesa Chacha amefafanua kuwa Chuo hicho kilizalisha mita 100, za majaribio na wamekubaliana na AUWSA kuanza kuzalisha mita hizo pia Chuo hicho linatoa ushauri wa kitaalamu kwa wanaojenga majengo ya kudumu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Chuo cha ufundi Arusha ,Dkt.Noel Mbonde amesema kuwa,chuo hicho kimekuwa kikifanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaandaa wanafunzi kuweza kujiajiri katika nafasi mbalimbali kutokana na mafunzo ambayo wamekuwa wakifundishwa kwa vitendo.