Naibu waziri wa Nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI Dkt Festo John Dugange wakati akizungumza katika hafla ya utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa soko kuu la mazao Manispaa ya Sumbawanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Pendo Mangali wakati akisaini mkataba wa ujenzi wa soko kuu la mazao eneo la Kanondo kupitia mradi wa uboreshaji miji Tanzania Tactic.
………………
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo John Dugange, amewataka viongozi wa serikali kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.
Dkt. Dugange alitoa wito huo leo, Desemba 6, 2024, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa soko kuu la mazao eneo la Kanondo, Kata ya Ntendo, kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC), katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Alisema kuwa kukamilika kwa soko hilo kutawezesha wafanyabiashara kuuza na kununua bidhaa mbalimbali, hatua ambayo itachangia Halmashauri hiyo kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kwa mwaka.
“Soko hili ni sehemu ya mradi unaotekelezwa katika miji mitano, manispaa 16, na mikoa 24. Jumla ya gharama za miradi yote ni Dola za Kimarekani milioni 410, sawa na shilingi trilioni 1.1 za Kitanzania. Mkoa wa Rukwa umepokea shilingi bilioni 7.3 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu,” alisema Dkt. Dugange.
Aliwataka wakandarasi wazawa kufanya kazi kwa weledi, uzalendo, na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati huku wakizingatia thamani ya fedha. Vilevile, aliagiza Halmashauri kote nchini kuhakikisha wananchi wanaelimishwa juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya miradi hiyo