Madaktari wa Tanzania wamehitimisha KambiTiba nchini Comoro kwa kutoa huduma kwa wagonjwa 2770 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa 7 ambapo wameweza kubaini wagonjwa takriban 269 wanahitaji rufaa za matibabu zaidi nje ya nchi na pia kuainisha fursa zaidi za ushirikiano katika sekta ya Afya.
Akizungumza katika hafla ya kuagana baada ya kuhitimisha KambiTiba hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete aliyekuwa Mkuu wa Msafari huo,Dkt Peter Kisenge amesema kuwa Kambi hiyo imekuwa na ufanisi mkubwa na muitikio kutoka kwa wananchi wa Comoro umekuwa mkubwa ambapo waliojitokeza walikuwa ni wengi kuliko walioweza kupata huduma licha ya madaktari hao kulazimika kufanya kazi hadi usiku wakati mwingine,”tumeweza kubaini uhitaji mkubwa wa huduma zetu na wapo ambao tumeona wanalazimika kupata rufaa kwa uangalizi zaidi,tumekubaliana na wenzetu wa hospitali ya El Maarouf kuwa KambiTiba hii iwemo katika kalenda zetu za vipaumbele na pia tujenge mfumo bora wa kisasa wa rufaa za matibabu kwa wanaokuja Tanzania ili wakija nchini kwetu kusiwe na kadhia wanazopata na wawe wanajua kabisa utaratibu wa kufuata na pia tumebaini maeneo muhimu ya kushirikiana zaidi hususan katika kuleta wataalamu wa fani mbali mbali washirikiane na wenzao” alisema Dkt Kisenge.JKCI ilikuwa ndio taasisi iliyoratibu Kambi hiyo.
Dkt Kisenge pia alieleza mazungumzo waliyofanya na Waziri wa Afya,Dkt Nassuha Ousseni Salim kuwa yametoa mwelekeo mzuri wa azma ya Serikali ya Comoro kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo kadhaa ikiwemo utoaji wa matibabu toka masafa ya mbali(Telemedicine) ambalo baadhi ya Taasisi za Tanzania wanaweza kutoa.
Kambi hiyo iliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro ilishirikisha Taasisi za JKCI,Tassisi ya Mifupa na Ubongo ya Muhimbili(MOI),Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mgeni Rasmi katika hafla ya kuwaaga madaktari hao alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Comoro,Youssoufa Mohamed Ali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala – CRC na Katibu wa Rais wa Nchi hiyo na kuhudhuriwa pia na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa,Shirika la Afya Duniani na Mabalozi wa Libya na Saudi Arabia.