Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekabidhi jumla ya shilingi milioni 360 kwa vikundi 53 kama mikopo isiyo na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani, ikiwalenga wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Mhe. Kemirembe Lwota, amewaonya wanufaika wa mikopo hiyo dhidi ya kutumia fedha hizo kwa starehe badala ya kuwekeza katika miradi inayolenga kukuza uchumi wao.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi hivyo, Mhe. Lwota alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10, na akasisitiza umuhimu wa kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Msigawane fedha hizi kwa matumizi yenu binafsi. Zitumikeni kulingana na maandiko ya miradi yenu ili kufanikisha malengo ya kuboresha maisha kupitia biashara. Onesheni kwa vitendo kuwa mikopo hii inamanufaa,” alisema Mhe. Lwota.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ndg. Mujibu Babara, aliwakumbusha wanufaika kuhusu viapo walivyoapa wakati wa kupokea mikopo hiyo na akasisitiza nidhamu ya fedha.
“Bila nyinyi kurejesha mikopo hii, itakuwa vigumu kwa wengine kupata nafasi ya kukopeshwa. Hakikisheni mnarejesha kwa wakati kama kanuni zinavyotaka,” alisema Babara.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kurudisha mpango huu wa mikopo na wakaahidi kutumia fedha hizo kujiinua kiuchumi kupitia miradi yenye tija ili waweze kurejesha mikopo kwa wakati.
Katika awamu hii ya kwanza, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imetenga shilingi milioni 360, ambapo vikundi 53 vimenufaika na fedha hizo. Mikopo hiyo, ambayo haina riba, inalenga kuwasaidia wanufaika kuanzisha na kukuza biashara kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.