Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza jambo leo Disemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo yamebeba kauli mbiu “Sera ya ushindani na kudhibiti kukosekana kwa usawa katika uchumi”
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wafanyabishara kuchangamkia fursa za masoko katika nchi mbalimbali Duniani kwa kuzalisha bidhaa zenye bora ambazo zinauwezo wa kushindana sokoni jambo ambalo litasaidia kuleta tija katika uchumi wa Tanzania.
Akizungumza leo Disemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo yamebeba kauli mbiu “Sera ya ushindani na kudhibiti kukosekana kwa usawa katika uchumi” Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Jafo, amesema kuwa Tanzania bado tunakazi kubwa ya kutengeneza bidhaa zenye ubora itakayoweza kushindana katika masoko ili kukuza uchumi wetu.
Dkt. Jafo amesema kuwa Tanzania ina fursa ya kuuza bidhaa katika masoko ya Nchi mbalimbali ikiwemo bara la ulaya pamoja china lakini bado kuchangamoto ya uwezo wa kuzalisha bidhaa za kutosha.
Amesema kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi ni dola milioni 85 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na nchi nyengine ikiwemo Afrika Kusini ambayo inauza dola bilioni 2.6.
“Miongoni mwa masoko ambayo ni fursa kwa watanzania ni pamoja na soko huru la Afrika ambapo wafanyabiashara wanaweza kufanya biashara nchi zaidi ya 50” amesema Dkt. Jafo.
Amesema kuwa masuala ya ushindani yanasaidia kupata bidhaa iliyokuwa bora, huku akieleza kuwa tukizalisha bidhaa ambazo hazina ubora upatikanaji wa fursa utakuwa ni mdogo katika kufanya biashara.
Dkt. Jafo ameipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa kuweka utaratibu rafiki wa kuadhimisha Siku ya Ushindani Duniani kwa kuwakutanisha wataalamu pamoja na wanafunzi kwa ajili ya kubadilishana maarifa na uzoefu katika maeneo mbalimbali ya ushindani.
Hata hivyo ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya tathmini kama kuna changamoto yoyote ya kisheria amabayo inakwamisha wafanyabiashara na kusababisha kushindwa kushiriki vizuri upande wa ushindani kwa ajili ya kutatuliwa.
“Serikali imeendelea kutengeneza fursa za uwekezaji ili wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa hiyo, taasisi nyingi za umma ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zimekuboresha mifumo yake kwa kuweke dirisha maalumu la kusajili biashara” amesema Dkt. Jafo.
Mwenyekiti wa Bodi Tume ya Ushindani (FCC) Dkt. Aggrey Mlimuka, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha soko linabaki shindani ili walaji waendelee kunufaika na ushindani katika soko.
Dkt. Mlimuka amesema kuwa wanaendelea na utekelezaji katika sera na sheria kwa kuzingatia msingi ili kuhakikisha washindani wote wanapata fursa sawa za kushindana kuuza bidhaa na kutoa huduma katika soko bila uwepo wa vikwanzo ambavyo vinasababisha kutoka katika soko.
“FCC inaendelea kuimarisha utendaji katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali pamoja na kushughulikia msingi ya ushindani katika soko” amesema Dkt. Mlimuka.
Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, amesema kuwa FCC wanatumia sheria na sera katika fursa ya ushiriki katika shughuli za uwekezaji na biashara zinafanyika kwa uweledi.
Amesema kuwa katika maadhimisho hayo wanaamini watapata maoni ya wadau kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu ambayo yatakwenda kuwasaidia katika utekelezaji.
“Haya ni maadhimisho ya kwanza ya siku ya Ushindani Duniani tangu marekebisho ya sheria ushindani nchini yalipofanyika, hivyo tunaamini yanakwenda kuleta tija” amesema Erio.