Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji Kopro Brian wakati akizungumza na wanafunzi katika shule ya Secondari ya Sumbawanga.
Afisa Uhusiano wa huduma kwa wateja Angeline Bidya wakati akizindua kampeni ya Umeme salama katika shule ya Sekondari ya Sumbawanga
Baadhi ya wanafunzi wakati wakiuliza maswali na kujibu
…………….
Shirika la umeme Tanzania TANESCO mkoa wa Rukwa limewataka wanafunzi kuacha tabia ya kuchezea na kuchuna nyaya za umeme.
Hayo yamesemwa na Ofisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo Angeline Bidya wakati akizindua kampeni ya kutoa elimu ya UMEME SALAMA mashuleni kwa kuanzia na Shule ya Sekondari Sumbawanga.
Akiwa ameambatana na timu ya watoa huduma kwa wateja Bidya ambae ni Mkuu wa kitengo hicho amesema elimu ya umeme salama kwa wanafunzi ni muhimu kwa usalama wao pindi wanapokuwa shuleni hata nyumbani.
“Elimu hii itawasaidia wanafunzi kuwa waangalifu wanapoona nyaya za umeme njiani na mahali popote na watajua Nini Cha kufanya baada ya kuona nyaya zimedondoka chini kwani hawatakiwi kuzigusa”.
Timu ya watoa huduma kwa wateja imehusisha pia Afisa Huduma kwa Wateja Bi. Zawadi Mgeni, Fundi Daniel Senga pamoja na maafisa kutoka Zimamoto.
Timu hiyo ilifika shuleni hapo kwa lengo la kuwapa wanafunzi elimu kuhusu usalama wa umeme, matumizi bora ya nishati, na hatua za kujilinda dhidi ya athari za matumizi mabaya ya umeme.
Akizungumza na wanafunzi hao Leo Dec 5 2024 Angeline ameeleza majukumu ya Tanesco kwa kuwaeleza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa.
Pia alieleza faida za kutumia mfumo wa kidijitali wa NIKONEKT, ambao unawawezesha wateja kupata huduma za umeme kwa urahisi bila kufika ofisi za TANESCO .
Aidha Angeline amewasisitizia kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi na salama ya umeme katika kuboresha maisha na maendeleo ya jamii kwa kufanya shughuli za kiuchumi ambazo zitawaingizia kipato .
Daniel Senga ambaye ni fundi ameonya kuhusu athari za matumizi mabaya ya umeme, ikiwa ni pamoja na hatari za shoti za umeme, vifo, na moto.
Ametoa wito kwa wanafunzi kuwa makini na kuhakikisha mifumo ya umeme shuleni na nyumbani inatumika kwa njia zilizo salama.
Kwa upande wake Afisa wa jeshi la zimamoto na uokoaji , Kopro Brian John amewaeleza kuhusu vyanzo vya moto mashuleni na mbinu za kuzuia ajali hizo.
Alisisitiza umuhimu wa kutochuna nyaya za umeme mabwenini kwa lengo la kuchaji simu au kuchemsha maji kwa kutumia majagi ya umeme, kwani vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa.
“Hii ni shule, na mmekuja kusoma Simu na majagi ya umeme hayana nafasi hapa” Alifafanua
Baadhi ya Wanafunzi akiwemo Janet Mwakasumba na Prosper Daniel walionyesha kufurahia elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wa usalama wa umeme kwa kufuata kauli mbiu ya kampeni Isemayo
*UMEME SALAMA, ELIMU YAKO, USALAMA WETU*
Hata Hivyo kampeni hiyo ilihitimishwa kwa maswali na majibu ambapo wanafunzi waliojibu vyema walipewa madaftari yenye ujumbe wa usalama wa umeme ili kuendelea kuielimisha jamii.