Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb),ameshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano baina ya Tanzania na UAE yaliyoandaliwa na Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash cha nchi hiyo.
Akizungumza mbele ya wanafunzi na wahadhiri wa Chuo hicho, Mhe. Waziri Kombo alitoa rai ya kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na UAE na kuweka misingi imara ya Kidiplomasia kwa vizazi vijavyo.
Kupitia mazungumzo yake chuoni hapo, Mhe. Waziri aliwasilisha salamu za pongezi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Mtawala wa Abu Dhabi Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan na wananchi wa UAE kote duniani kwa kuadhimisha miaka 53 ya siku adhimu ya Taifa lao.
Mhe. Kombo amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zina historia ndefu ya urafiki na uhusiano tangu enzi za biashara za Ghuba ya Uajemi kupitia Bahari ya Hindi hadi mwambao wa Tanzania, kuanzia Zanzibar, Dar es Salaam hadi Mtwara.
“Msingi imara uliowekwa na waasisi wa mataifa haya, marehemu Sheikh Zayed bin Sultan al Nahyan na hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania na UAE ziliimarisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1974 baada ya kuungana kwa UAE mwaka 1971, “ alisema Balozi Kombo.
Ameongeza kuwa uhusiano huo umeendelea kuwa wa kirafiki na wenye mshikamano tangu wakati huo na kwamba anaamini kuwa uhusiano huo utaimarika zaidi katika miaka mingi ijayo.
Mhe. Waziri Kombo ametumia mhadhara huo kunadi fursa za biashara, uwekezaji na Utalii zilizopo nchini na kuwaita wananchi wa UAE kuja nchini kuwekeza na hivyo kuzinufaisha pande mbili kupitia Diplomasia ya Uchumi .
Akiongea kuhusu Ushirikiano na Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash amesema Chuo hicho kina uhusiano na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ambao mwezi huu umetimiza mwaka mmoja tangu kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyoanzisha uhusiano huo ambayo ilisainiwa mwezi Desemba 2023, wakati wa Mkutano wa COP28 uliofanyika Dubai.
“Kusainiwa kwa makubaliano hayo kunafanya kuwa chombo muhimu kinachochangia faida kubwa kwa ushirikiano uliopo, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kubadilishana uzoefu kati ya wakufunzi na wataalamu, kutoa mihadhara ya kidiplomasia, na kufanya utafiti wa pamoja kwenye maeneo kama utatuzi wa migogoro, diplomasia ya kiuchumi, na mengineyo,” alisema Balozi Kombo.
Pia alitumia mhadhara huo kukishukuru Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa Maafisa wa Wizara kuhudhuria kozi fupi ya diplomasia katika Chuo hicho mwaka huu ambapo maafisa hao wanasubiri tarehe ya kuanza kozi na kuongeza kuwa ni matumaini yake kuwa Chuo hicho pia kitakuja nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania.
Alisema ni imani yake kuwa mafunzo hayo yatawajengea watumishi hao wa Wizara ujuzi wa vitendo na uzoefu unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao na kukuza taaluma zao.
Balozi Kombo yuko nchini UAE kuhudhuria majadiliano ya kwanza ya kisiasa na Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE ambapo pia ameshiriki katika maadhimisho ya miaka 53 ya Taifa la UAE yaliyofanyika Desemba 2, 2024.