Sheikh Hasani Kabeke pia Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, leo akisistiza jamboh alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwakwe.Picha na Baltazar Mashaka.
……….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA),Mkoa wa Mwanza limeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita,kwa kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 kwa weledi vikiwemo vyama vya siasa kukubali matokeo na kuufanya umalizike kwa amani.
BAKWATA pia,katika kuadhimisha Siku ya Maulid itakayofanyika kimkoa katika Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Magu,imeiagiza misikiti yote mkoani Mwanza,kufanya dua maalum kwa ajili ya wazee,waliojitoa kupigania Uhuru wa nchi yetu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke amesema, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27,mwaka huu,ulifanyika kwa amani na utulivu na kutuvusha salama.
“BAKWATA linaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,naipongeza kwa sababu mtakumbuka Novemba 27,2024,tulikuwa na zoezi la kihistoria,Uhuru linaloonesha sisi ni binadamu na tunajitambua,limeonesha Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba na utawala wa sheria,”amesema.
Sheikhe Kabeke pia ametoa wito kwa Watanzania kuwa baada ya uchaguzi waendelee kuiombea nchi yetu baraka,amani,utulivu na mshikamano,bila amani maendeleo yote anayohangaikia Rais Dk.Samia hatayakuwa na manufaa wala faida.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema fursa hiyo waliyopewa Watanzania ya kuwachagua viongozi wao wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji ilikuwa nzuri kuanzia uandikishaji,namna wananchi walivyohamasishwa na kuhimizwa kushiriki uchaguzi kwa amani.
Amesema viongozi wa dini kushirikishwa,wakapewa elimu wakasaidia kuhamasisha jamii kujiandikisha hadi kupiga kura,mkoani Mwanza ilishududiwa amani ikitawala na ndio sababu ya kuishukuru serikali.
Sheikh Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini amevishukuru vyama vya siasa kwa kuonesha utulivu,kwani watu walidhani kungetokea viashiria vya uvunjifu wa amani wakati wa kutangaza matokeo.
Amesema viongozi wa dini wanashukuru kwa mahubiri yao,maelekezo na wosia wao kwa Watanzania kuwa,atakayebahatika kuchaguliwa apokee kwa heshima ushindi,ambaye kura hazikutosha akubali matokeo na amshukuru Mwenyezi Mungu ajipange kwa wakati mwingine.
“Tumevuka salama na vyama vyote vilikuwa vitulivu na tumepokea kwa heshima,nivipongeze vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi wamefanya kazi nzuri na kwa weledi, vyombo vya ulinzi na usalama pia vilifanya nzuri Mwanza imekuwa tulivu na imevuka salama,”amesema Sheikh Kabeke.
Akizungumzia Sherehe za Maulidi zitakazofanyika Disemba 8, mwaka huu,Msikiti Mkuu wilayani Magu,amesema adhuhuri ya siku hiyo misikiti yote mkoani Mwanza,ifanye dua maalumu ya kumuombea Rais Samia ikiwemo kuiombea nchi amani na wazee waliojitoa kupigania Uhuru.
Amevishukuru vyombo vya habari kwa kuwa sehemu ya BAKWATA katika kufikisha habari katika jamii,vimeisaidia kufahamu mambo mengi yakiwemo maendeleo na harakati za taasisi hiyo ya dini na kusisitiza maendeleo ya BAKWATA yana mchango mkubwa wa waandishi wa habari.
Katika hatua nyingine BAKWATA imelaani matukio ya ukatili yakiwemo ya ulawiti,ubakaji,mauaji na unyanyasaji wa kijinsia na kuwataka viongozi na wamiliki wa madrasa na markazi kuzisiamamia kwa weledi zisiwe chanzo cha matukio hayo mabaya katika jamii.
Pia,taasisi hiyo itatumia sherehe za Maulidi kupanda miti ili kutunza na kulinda mazingira,kuchangia damu kwa ajili ya kusaidia hospitali na vituo vya afya,akiba ya damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji ikizingatia damu haina kiwanda.