Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Uelewa Mdogo Juu ya Magonjwa Yasiyoambukiza Wahitaji Kuongezwa
Magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, na saratani ni miongoni mwa magonjwa hatari yasiyoambukiza, lakini uelewa mdogo kuhusu magonjwa haya umeendelea kuchangia ongezeko la wagonjwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii ya Same. Katika kipindi cha miezi 10 ya mwaka 2024, kuanzia Januari hadi Oktoba 30, wagonjwa 200,391 waliotembelea vituo mbalimbali vya afya, ambapo 10,089 (5.03%) walikuwa na shinikizo la juu la damu (Hypertension), 3,885 (1.9%) walikuwa na ugonjwa wa kisukari (Diabetes Mellitus), na 124 (0.01%) walikuwa na saratani za aina mbalimbali.
Dkt. Alexander alieleza kuwa hali hii inatokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo, jambo linalochangia ongezeko la idadi ya wagonjwa, na mara nyingine magonjwa haya husababisha vifo.
Ili kuleta mabadiliko, Kampuni ya Mtabe Group Tz Limited kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), wameendesha kambi ya kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa magonjwa yasioambukiza pamoja na kutoa elimu kwa wakazi wa Kata ya Hedaru.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma hizo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alishukuru Kampuni ya Mtabe Group Tz Limited kwa kuchangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa huduma hizi muhimu kwa wakazi wa Hedaru. Kasilda alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hii kupata huduma za uchunguzi na kujua hali zao za afya.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa ni muhimu kwa jamii kuzingatia maisha bora, ikiwa ni pamoja na kula ulaji unaofaa, kuepuka msongo wa mawazo, na kufanya mazoezi mara kwa mara. Alisema kuwa magonjwa mengi yasiyoambukiza yanaweza kuzuilika kwa kuwa na mtindo bora wa maisha.
“Serikali pekee haiwezi kutatua changamoto hizi, ni lazima tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa haya,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mtabe Group Tz Limited, Jerald Agrey, alisema kuwa kampuni yao imeguswa na hali ya jamii na ndiyo maana wameamua kuanzisha zoezi hili la kutoa huduma na elimu kwa umma. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kuwa na uelewa wa pamoja ili kupambana na magonjwa yasioambukiza, kwani serikali pekee haiwezi kufanya mambo yote kwa wakati mmoja.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha jamii inapata ufanisi katika kuzuia magonjwa haya. Huu ni mchango wetu katika kuhakikisha wananchi wa Same wanaishi kwa afya njema,” alisema Agrey.