*Serikali kufikisha umeme vitongoji vilivyobaki
*Asisitiza Serikali inatambua mchango wa wadau wa maendeleo
Monduli Arusha
Serikali imeahidi kufikisha umeme katika Shule ya Msingi ya Lucas Mhina ili wanafunzi na wanakijiji wapate nishati ya umeme itakayowawezesha kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii.
Hayo yamebainishwa leo Disemba 3, 2024 na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alipotembelea miradi inayotekelezwa na Sekta ya Nishati katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 ili kufikisha umeme katika Shule ya Msingi Lucas Mhina ili wanafunzi waweze kutumia umeme katika masomo yao, ” amesema Mhe. Kapinga.
Mhe. Kapinga ameielekeza TANESCO kuhakikisha inafikisha umeme katika shule hiyo kwa kuwa Serikali imetoa fedha ya ya mradi huo.
Katika hatua nyingine, amesisitiza kuwa, Serikali itafikisha umeme katika vitongoji vilivyobaki nchini ili kukuza uchumi wa wananchi na Pato la Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema, Wilaya ya Monduli ina jumla ya kata 20, vijiji 62 na vitongoji 236 ambapo vijiji vyote tayari vimefikiwa na huduma ya umeme sawa na asilimia 100.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Idara ya Umeme Vijijini, Mha. Romanus Lwena amesema wakala unaendelea na utekelezaji wa upelekaji wa umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobaki ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.