Mwamvua Mwinyi, Pwani 3, Disemba 2024
Kiwanda cha KEDA (T) Ceramic Co. Ltd kimekamilisha ujenzi wa daraja katika Mto Msorwa, barabara ya Mbezi-Msorwa-Shungubweni-Boza, lililogharimu milioni 150 ili kuunganisha maeneo hayo.
Mradi huo umetokana na mpango wa Kiwanda cha KEDA wa kurudisha fadhila kwa jamii pamoja na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanaonufaika na uwekezaji kwenye maeneo yao.
Akizungumza katika eneo la mradi, Afisa Biashara wa kiwanda cha KEDA, Masoud Suleyman, alisema uboreshaji wa miundombinu hiyo utarahisisha shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii kwa wakazi wa kata hizo.
Pia, barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa malighafi ya mchanga inayotumika katika utengenezaji wa bidhaa za vioo.
“Daraja lina urefu wa mita 6, upana wa mita 7, na kina cha mita 1.5 , Mradi umetumia gharama ya sh. milioni 150, fedha zilizotolewa kama ufadhili wa kiwanda cha KEDA kwa mwaka 2024.”
” Utekelezaji umeanza tarehe 28 Oktoba 2024 kwa kushirikiana na wataalamu wa TARURA Wilaya ya Mkuranga, huku vifaa na malighafi zote zikitolewa na KEDA,” alisema Suleyman.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameeleza furaha yao kwa kukamilika kwa daraja hilo akiwemo Mohammed Msumi, mkazi wa kitongoji cha Kikopi.
Kikopi alisema , hapo awali walikuwa wakipata tabu kuvuka eneo hilo, hasa wakati wa mvua.
“Vijana walikuwa wakivusha watu kwa malipo, Lakini sasa, KEDA wamejenga daraja lenye ubora wa hali ya juu.”Tunawashukuru kwa ukarimu wao na tunawakaribisha wawekezaji wengine kuendelea kusaidia,” alisema Msumi.
Amina Mohammed Juma naye alisema daraja hilo limeondoa changamoto ya magari kukwama wakati wa mvua, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kisayani, Jumanne Mtambwe, alifafanua mradi huu umeleta chachu ya maendeleo kwa kuwa sasa barabara zinapitika kwa urahisi.
Tunawashukuru KEDA, lakini pia tunaomba wajenge barabara kwa kuwa magari yanayobeba mchanga, ambayo ni malighafi muhimu kwa kiwanda, yanaisababisha kuharibika,” alisema Mtambwe.