Mwenyekiti wa(TVA),Profesa Esron Karimuribo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo mkoani Arusha
Katibu Msaidizi wa TVA na Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Dkt Caroline Uronu akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Sayansi cha Nelson Mandela cha Mkoani Arusha,Dkt Gabriel Shirima akizungumza kuhusu mkutano huo
……….
Happy Lazaro, Arusha
Kongamano la kisayansi la 42 na mkutano mkuu wa Chama cha Kitaaluma cha Kisayansi cha madaktari wa wanyama Tanzania (TVA) unaotarajiwa kufanyika mkoani Arusha kesho ukiwa na malengo ya kuzungumza namna ya kutokomeza magonjwa ya Mifugo ili kuongeza tija ya uzalishaji .
Aidha madhumuni mengine ni pamoja na kuimarisha biashara ya Mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi .
Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Mwenyekiti wa(TVA),Profesa Esron Karimuribo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo ambao unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha Prof . Karimuribo amewataka kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatokomeza magonjwa ya mifugo hapa nchini ili mifugo iweze kuuzwa nje ya nchi na serikali kuongeza pato la nchi.
Aidha amesema kuwa katika miaka ya 1970 hadi mwaka 1980 mifugo ilikuwa ikikabiliwa na magonjwa mengi sana lakini hali hiyo imebadilika na magonjwa yote ya kuambukiza yametokomezwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na madaktari wa Mifugo kwani kwa sasa wapo madaktari wa kutosha kila mahali mpaka vijijini.
Ameongeza kuwa TVA imekuwa ikishirikiana na serikali katika kukabiliana na magonjwa ya mifugo na kufikia hatua sasa mifugo ya hapa nchini kukubalika kuuzwa nje ya nchi na kuingizia serikali mapato na fedha za kigeni.
Hata hivyo ameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kuongeza bajeti Wizara ya Mifugo na Uvuvi hadi kufikia shilingi Bilioni 460 na hiyo inawapa nguvu wataalamu kufanya kazi katika mazingira mazuri yenye kuisaidia nchi kutoka ilipo na kusonga mbele.
Profesa Karimuribo amesema serikali imetenga shilingi Bilioni 28 kwa ajili ya chanjo ya mifugo hiyo imewapa moyo na nguvu wataalamu wa mifugo kuona kuwa idara hiyo inapewa kipaumbele katika kuhakikisha magonjwa ya mifugo nay a mlipuko yanathibitiwa kwa maslahi ya nchi na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa TVA Caroline Uronu amesema kuwa Chama hicho ni mmoja ya vyama vya kitaalamu vikongwe nchini na kinatambulika serikalini na kinaisaidia sana serikali hususani Wizara Mifugo na Uvuvi katika kupambana na magonjwa ya mifugo na kuthibiti magonjwa ya milipuko.
Uronu amesema kuwa Madaktari wa Mifugo waliopo katika TVA wamesambaa katika maeneo mbali mbali nchini ikiwemo Wizara ya TAMISEMI lengo likiwa moja kuhakikisha mifugo yote nchini inakuwa salama kwa maslahi ya nchi.
Naye Mhadhiri wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ,Dkt Gabriel Shirima amesema kuwa ubora wa Mifugo na Wanyama ikiwa salama na afya ya binadamu inakuwa salama na uwezekano wa ongezeko la mifugo na wanyama ikawa kubwa na nchi kuongeza mapato.
Aidha kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 2000 nchini na Wataalamu kutoka Jumuiya ya Madola wamealikwa katika Kongamano hilo lengo ni kutaka kuhakikisha Tanzania na Afrika inakuwa na Mifugo na Wanyama yenye ubora uliotukuka na uliozingatia afya bora ili mifugo hiyo iweze kuuzwa nje.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha TVA kwa kushirikiana na Chama cha wasaidizi wa madaktari wa wanyama Tanzania (TAVEPA) na Chama cha madaktari wa wanyama wa jumuiya ya Madola (CVA).