Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mkoani Mbeya maeneo ya Soweto.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Letshego Faidika, Bw Baraka Munisi akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mkoani Mbeya maeneo ya Soweto.
Mjumbe wa bodi wa Benki ya Letshego Faidika, Bw Adam Mayingu akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mkoani Mbeya maeneo ya Soweto.
Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa (wa tatu kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Letshego Faidika Bw Baraka Munisi (wa tatu kushoto) na Mjumbe wa bodi wa benki ya Letshego Faidika, Adam Mayingu (wa pili kushoto) wakishiriki katika uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mkoani Mbeya. Tawi hilo lipo eneo la Soweto.
Mkurugenzi wa Benki Kuu tawi la Mbeya Dkt. James Machemba akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Letshego Faidika lililopo eneo la Soweto mkoani Mbeya.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa benki ya Letshego Faidika Bw. Asupya Nalingigwa (katikati) na Mshirika wa Biashara wa Masoko na Mawasiliano Bi. Valdy Khahima wa benki ya Letshego Faidika (wa kwanza kulia) na Devotha, Afisa Utawala wa Wilaya wakiwa katika majadiliano wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Letshego Faidika lililopo eneo la Soweto mkoani Mbeya.
…………………
Na Mwandishi wetu
Mbeya. Benki ya Letshego Faidika imetumia jumla ya Sh 5,348,067,950.91 kukopesha wateja 1,305 wa mkoa wa Mbeya.
Hayo yamesemwa na mjumbe wa Bodi ya Benki ya Letshego Faidika, Bw Adam Mayingu wakati wa ufunguzi wa taji jipya la benki hiyo maeneo ya Soweto mkoani Mbeya.
Awali tawi hilo lilikuwepo kwenye Jengo la Royal Zambezi kabla ya kuhamia Soweto, karibu na barabara ya Moondust.
Bw Mayingu amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kimekopeshwa kwa wateja wao mbalimbali serikalini na sekta binafsi.
Amesema kuwa Benki ya Letshego Faidika ni matokeo ya muungano kati ya taasisi ndogo ya kifedha, Faidika, na Benki ya Letshego Tanzania ambayo ilianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka jana.
Alisema kuwa tawi la mkoa wa Mbeya lina historia ya kipekee ambapo kwa upande wa Benki ya Letshego ilianza kutoa huduma mwaka 2016 na kwa upande wa Faidika ulianza kutoa huduma mwaka 2008.
“Mpaka sasa tumeweza kuwahudumia wateja zaidi ya 3,417 kwa Mkoa wa Mbeya pekee. Pia, tuna satellite 6 ambazo ziko Ileje, Mkwajuni, Mbarali, Tukuyu, Kyela, na Mbozi. Tunalojivunia sana, kwani linaleta uthibitisho wa dhamira yetu ya kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi Mbeya na mikoa mengine,”alisema Bw Mayingu.
Alisisitiza kuwa huduma za benki hiyo zinalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa suluhisho la kifedha kwa watumishi wa umma, wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo na wa kati, na huduma nyingine kama mikopo ya magari, akaunti za akiba, na bima.
“Kauli mbiu yetu, “Tunaboresha Maisha,” inaendelea kuimarisha dhamira yetu ya kuwa washirika wa kweli wa maendeleo.
Kwa mara nyingine tena, napenda kutoa pongezi za dhati kwa timu ya Letshego Faidika kwa kazi kubwa ya kuandaa uzinduzi huu. Pia, niwashukuru washiriki wote wa kikundi kazi kilichoshiriki kuhakikisha kuwa uzinduzi huu unafanikiwa.
Tunatarajia kuendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuhakikisha huduma bora na zenye tija zinaendelea kupatikana hapa Mbeya.
Ni matumaini yangu ni kuwa tawi hili jipya litakuwa daraja muhimu katika kufikia malengo yetu ya maendeleo kwa jamii ya Mbeya na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Kwa upande wake,mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa aliipongeza benki hiyo kwa kufungua tawi hilo huku akiiomba kuongeza matawi zaidi mkoani humo na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Malisa alisema kuwa Mbeya ni mlango wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ni fursa kwa benki hiyo kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika mikoa ya kusini.
Alisema kuwa asilimia 95 ya wakazi wa mkoa wa Mbeya ni wafanyabiashara ambapo endapo benki ya Letshego Faidika ikiwatumia vizuri, watapata faida kubwa.
Mheshimiwa Malisa pia alitao wito kwa viongozi wa benki hiyo kuendelea kupanua wigo wa huduma kwa kufungua matawi zaidi, ili kuwafikia wateja zaidi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Mbeya.
“Ni wazi kuwa wafanyabiashara ndiyo wakopaji wakubwa katika benki mbalimbali kwa lengo la kukuza mtaji. Hivyo mkoa wa Mbeya una fursa kubwa na naomba uongozi wa benki kuangalia uwezekano wa kuongeza mitawi zaidi na vile vile kuongeza muda wa kufanya kazi kwa siku za mbele hadi masaa 24.
Naipongeza benki kwa kutoa elimu katika huduma ya mikopo kwa wateja kabla ya kukopa kwa lengo la kuwawezesha wateja kutukia mikopo hiyo kwa maendeleo,” alisema Mheshimiwa Malisa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Benki Kuu tawi la Mbeya, Dkt. James Machemba alisema aliipongezabenki hiyo kwa huduma bora za kifedha nchini na pia pia kuendelea kupanua wigo wa huduma za kibenki.
Alisema kuwa kufungua tawi mkoani humo, kuleta ushindani na benki nyingine ili kuwapa chagua wateja.