Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya Kufunga Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika Sherehe ya Kufunga Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Sherehe ya Kufunga Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Usshirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (wa pili kutoka kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CEO Roundtable of Tanzania Bw.David Tarimo (wa pili kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya CEO Roundtable of Tanzania mara baada ya sherehe ya Kufunga Mwaka ya Taasisi hiyo iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CEO Roundtable of Tanzania Bw. David Tarimo mara baada ya sherehe ya Kufunga Mwaka ya Taasisi hiyo iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wanachama wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kuvumbua njia zinazotekelezeka katika kuhamisha teknolojia zitakazowasaidia vijana ambao ni idadi kubwa ya Watanzania kwa sasa.
Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya Kufunga Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) iliyofanyika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam. Amesema ni muhimu kuwasaidia vijana katika teknolojia za kijani, kuunga mkono katika tafiti na maendeleo pamoja na kuanzisha vituo atamizi vya teknolojia.
Amewasihi kupitia upya vigezo vya kujiunga na CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) ili kuongeza idadi ya vijana kutoka biashara zinazochipukia kama vile masuala ya burudani, tehama na michezo.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kahamasisha wanachama wao kuipa kipaumbele ajenda ya mabadiliko ya tabianchi. Amewasihi kuongeza jitihada katika ushirikiano na suluhu za kibunifu ambazo zitahusianisha shughuli za Taasisi zao na malengo ya Taifa ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kutumia fursa zinazotokana na uhifadhi.
Vilevile Makamu wa Rais Amesema unahitajika ushirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika kutafuta mwelekeo sahihi kuelekea uchumi wa kijani ambao unaunga mkono maendeleo endelevu na kuendana na vipaumbele vya Taifa.
Pia, amesema wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana ikiwemo kubadili mitaala itakayowezesha kuendana na soko la ajira, CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) inapaswa kuongeza wigo wa shughuli zake ili kuongeza ajira zaidi, kutoa mafunzo kwa vitendo na mitaji kwa biashara zinazochipukia kwa wahitimu.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo mabadiliko ya sera na miundo ya kitaasisi ili kudhibiti urasimu pamoja na rushwa na hivyo kuchagiza sekta binafsi shindani. Ameongeza kwamba serikali imeimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhamasisha diplomasia ya uchumi ili kulifanya Taifa kuwa kiungo muhimu kikanda na kimataifa pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka mataifa ya nje. Ametoa wito wa kuongeza ushirikiano wa kibunifu baina sekta binafsi na serikali katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi wanachama wa CEO Roundtable of Tanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na Mkutano Mkubwa wa Nishati wa Wakuu wa Nchi (Heads of State Summit on Mission 300) utakaofanyika mwezi Januari 2025 hapa nchini. Amesema Mkutano huo unaoratibiwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika ni muhimu ukatumika kuangalia fursa ikiwemo kuingia makubaliano ya kibiashara , kujenga urafiki na kupata uzoefu kutoka katika mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayotarajiwa kushiriki.
CEO Roundtable of Tanzania inajumuisha Wakurugenzi na Watendaji Wakuu kutoka Makampuni zaidi ya 200 kutoka sekta mbalimbali nchini ambapo wanachama wake wanachangia katika maeneo ya kukuza na kuendeleza uchumi ikiwemo uchangiaji wa kodi na kuimarisha uongozi nchini kupitia programu za mafunzo.
Hafla ya Mwaka ya CEO Roundtable of Tanzania kwa mwaka 2024 imelenga kutafakari maono ya maendeleo yanayotarajiwa kufanikishwa ndani ya nchi katika kuelekea utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo ( Dira 2050) na mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha mpango huo.
Hafla hiyo iliyobeba kauli mbiu isemayo “Dira 2050…Twende zetu” imewakutanisha viongozi zaidi ya 200 kutoka Sekta Binafsi, Serikali na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kwa lengo la kutafakari mafanikio na changamoto za mwaka uliyopita na kuangazia ajenda za mwaka ujao.