Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kuthibitisha uimara wake katika uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma baada ya kushinda tuzo ya uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa viwango vya kimataifa kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Hii ni ishara ya kujituma kwa shirika hilo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji wa kifedha, ambapo imejipatia nafasi ya kwanza miongoni mwa Mamlaka 9 za Udhibiti zilizoshindanishwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo hiyo iliyofanyika tarehe 29 Novemba 2024, CPA Benjamin Mashauri, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuzingatia viwango vya kimataifa katika uandaaji wa taarifa za kifedha ili kuboresha utawala bora.
CPA Pascal Kalomba, Mkurugenzi wa Fedha wa TASAC, aliyetunukiwa tuzo hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Mohamed Salum, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi wa shirika hilo. “Hii inaonyesha dhamira yetu ya kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinasimamiwa kwa uwazi, uwajibikaji, na ufanisi,” alisema.
Kwa ushindi huu, TASAC imeweka alama muhimu siyo tu katika sekta ya usafiri wa majini, bali pia kama mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini. Mashindano hayo yalihusisha taasisi 86 za umma na binafsi, hatua inayotoa changamoto kwa mashirika mengine kufuata nyayo za TASAC katika kuimarisha mifumo ya uhasibu na utoaji wa ripoti kwa viwango vya kimataifa.