* Dkt.Biteko afungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa 7 wa AAAMA
* Awataka washiriki kubuni mbinu za kukabili changamoto zilizopo
* IMO yaahidi kuendeleza ushirikiano kukabiliana na changamoto Baharini
* Dar es Salaam yampongeza Rais Samia kuboresha Bandani, kupunguza msongamano
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri majini Barani Afrika zimetakiwa kushirikiana na kuungana ili kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji majini na hivyo kuchochea maendeleo ya Uchumi katika nchi husika.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (Novemba 29, 2024) wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukumuiya ya Mamlaka za Usimamizi na Usafirishaji Majini Barani Afrika unaofanyika kwa siku tatu, Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amewashauri washiriki kutumia mkutano huo kama fursa ya kubuni na kupanga mikakati mipya ya kuelekea katika mafanikio kupitia sekta hiyo ambapo amesisitiza kuwa ushirikiano miongoni mwa washiriki na kujadiliano juu ya kuwezesha masuala mbalimbali na sekta ya usafirishaji litakuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zilizopo.
“Kila mmoja wetu atumie fursa ya mkutano huu kujiwekea malengo yatakayo tuwezesha kufikia azima ya kuboresha usalama na kuimarisha sekta ya usafirishaji wa majini” amesema Dkt. Biteko.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema miongoni masuala yanayohitaji kutiliwa mkazo ni pamoja na suala la raslimali watu hususan vijana amabo watachagiza uendelevu na ukuaji wa sekta ya usafiri na usalama wa usafirishaji wa majini.
Profesa Mbarawa amesema Tanzazania kwa upande wake imekuwa mstari imekuwa ikitekeleza maazimio ya uboreshaji wa sekta hiyo ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa inayolenga pamoja na mambo mengine, kupunguza uzalishaji wa hewa ya Kaboni
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Reli ya Umeme kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma mbali na kuongeza ufanisi katika usafirishaji, pia imepunguza uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Masuala ya Baharini (IMO), Arsenio Dominguez ameiopongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kongamano na Mkutano huo suala linaloonesha utayari wake katika uboreshaji wa sekta ya usafirishaji na usalama wa majini.
Dominguez amesema IMO itaendelea kuwezesha vikao hivyo vya kimataifa ili kujenga na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama ili kukabiliana na changamoto katika nchi husika.
Amesema IMO ina program nyingi zinazohusu hifadhi ya mazingira na uwezeshaji kuelekea usawa wa kijinsia ambapo amesema wanawake wako nyuma katika masuala ya usafirishaji na usalama majini.
Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kupunguza msongamano katika upakiaji na upakuaji wa mizigo Bandarini hapo.
“Tunaomba ufikishe salam hizo kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwambie tunamshukuru kwa huduma za uboreshaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam sasa hivi hatuna msongamano wakati wa kupakia au kupakua mizigo Bandarini, amesema Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.