Na Silivia Amandius – Kagera.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imekabidhi mbao 400 kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, kwa ajili ya kutengeneza mizinga ya nyuki katika maeneo maalum yatakayoainishwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mbao hizo kwa niaba ya Kamishna wa TFS, Mhifadhi Mwandamizi wa Wilaya ya Bukoba, Anatol Lagwen Qamara, alisema msaada huo unalenga kusaidia wananchi kuchonga mizinga ya nyuki ili kuinua uchumi wa jamii na kuhifadhi mazingira yanayowazunguka.
Kwa upande wake, Hajat Fatma Mwassa alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha uhifadhi endelevu wa mazingira. Ameahidi kuwa mizinga itatengenezwa na kugawiwa kwa wahusika katika maeneo yaliyotengwa, hatua ambayo itasaidia katika ufugaji wa nyuki kwa njia salama na endelevu huku ikizingatia utunzaji wa mazingira.