Na Silivia Amandius – Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amewataka wakazi wa mkoa huo kuendeleza utulivu na kufuata taratibu za uchaguzi baada ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo, Novemba 27, 2024.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Uwanja wa Ndege, mtaa wa Pwani, kata ya Miembeni, Hajjat Mwassa amesisitiza kuwa hakuna sababu ya vurugu, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinapingana na mila na desturi za wakazi wa Kagera.
“Mkoa wa Kagera unajulikana kwa ustaarabu, utulivu, busara, na hekima. Hatuwezi kuruhusu uchaguzi kuwa chanzo cha migogoro. Zoezi hili litamalizika salama,” alisema.
Akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wakiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Jocobo Nkwera, na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima, Mwassa ametembelea vituo kadhaa vya kupigia kura ikiwemo Kilima Hewa, Katatwolansi, Kashai Halisi, Miembeni, na Kahororo.
Mwassa alionesha kuridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi na kuwasihi wale ambao bado hawajapiga kura kufanya hivyo mapema ili kuchangia maendeleo ya jamii yao.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama imeimarishwa mkoa mzima, akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuchangia kudumisha amani.
“Nimefurahishwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza. Tunatarajia kumaliza zoezi hili kwa utulivu na ufanisi. Nawashauri wale waliobaki majumbani waje wapige kura ili kuleta mabadiliko chanya,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa, mkoa wa Kagera una zaidi ya wapiga kura milioni 1.5 waliotawanyika katika vituo 4,012 vya kupigia kura. Hadi sasa, zoezi la uchaguzi linaendelea kwa amani na utulivu.