Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu leo ametembelea hospitali kuu ya El Maaruf nchini humo na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo,Assoumany Abdou kuhusu ziara maalum ya madaktari na wataalam wa Afya 20 wanaokuja Comoro kufanya KambiTiba.
Balozi Yakubu alimueleza Mkurugenzi Mtendaji kuwa jumla ya Madaktari 16 na Wauguzi na Wataalam 4 watawasili nchini Comoro tarehe 28 Novemba,2024 na kuendesha Kambi Tiba itakayojumuisha uchunguzi wa magonjwa mbali mbali ikiwemo maradhi ya moyo,magoti,mgongo,ubongo,saratani,figo,mfumo wa chakula na matatizo ya mkojo na watakuwa nchini humo kwa wiki moja.
Aidha,Balozi Yakubu alimueleza kuwa wataalamu hao wanatoka hospitali za Muhimbili,Benjamin Mkapa na Taasisi ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete,Taasisi ya Saratani ya Ocean Road,Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) na wataalam toka Wizara ya Afya.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu Assoumany alimueleza utayari wa Hospitali yake na kuwa wanashukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa wataalam hao kuja nchini Comoro.