Afisa Mawasiliano na Tahadhari za Mapema kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Bi Rahma Vuai Sleiman akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Sheha katoka Shehia za Wilaya ya Mjini huko Skuli ya Sekondari Salim Turky Mpendae.
Abdullah Hussein Hamad kutoka Kampuni ya Ismail LPG Campany akielezea matumizi sahihi ya Majiko ya Gesi kwa Wajumbe wa Kamati za Sheha katoka Shehia za Wilaya ya Mjini huko Skuli ya Sekondari Salim Turky Mpendae.
Sheha wa Shehia ya Mtumwa Jeni Rajab Ally Ngauchwa akitoa shukrani kwa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar pamoja Ismail LPG Campany kwa kutoa mafunzo ya kukabiliana na Maafa ikiwemo matumizi bora ya Gesi ya kupikia huko Skuli ya Sekondari Salim Turky Mpendae.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Sheha kutoka Shehia za Wilaya ya Mjini wakisikiliza kwa makini Mfanyakazi wa Kampuni ya Ismail LPG Campany Abdullah Hussein Hamad (hayupo Pichani)katika Skuli ya Sekondari Salim Turky Mpendae.
…….
Wilaya ya Mjini.
Jamii Nchini imeshauriwa kuchukuwa tahadhari ya matumizi ya Nishati ya Umeme na Majiko ya Gesi ya kupikia ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Kauli hiyo ametolewa na Afisa Mawasiliano na Tahadhari za Mapema kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Bi Rahma Vuai Sleiman wakati akitoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati za Sheha katika Shehia za Wilaya ya Mjini huko Skuli ya Sekondari ya Salum Turky Mpendae.
Amesema baadhi ya ajali za Moto zinasababishwa na Majiko ya Gesi na Umeme jambo ambalo linaiathiri jamii kwa kukosa Makaazi na mahitaji muhimu ya kujikimu.
Aidha amewataka Wazazi na Walezi kuwasimamia Watoto wao wanapotumia Nishati hizo ili kuwaepusha na ajali zinazoweza kujitokeza.
Hata hivyo amesema katika msimu wa Mvua za vuli kumejitokeza Majanga mbalimbali yanayosababishwa na mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo Mafuriko kwa baadhi ya maeneo hasa ya Mabondeni,Mripuko wa Maradhi ya Matumbo , Upepo mkali ambao huezua mabati ya nyumba pamoja na kung’oka kwa Miti jambo ambalo linahitaji jamii kuchukuwa tahadhari ya kutosha.
Nae Afisa Maafa Wilaya ya Mjini Bi Pili Haji Foum amewataka Wajumbe hao kupanga Mikakati ya kukabiliana na Maafa katika shehia zao pamoja na kuziorodhesha sehemu zote hatarishi zilizopo katika maeneo yao.
Amesema kuwa iko haja ya Jamii kubadilika kutokana na Mazingira yaliopo kubakia na Fitting za Umeme za kizamani na badala yake kuweka za kisasa ambazo zinahimili umeme mkubwa pamoja na kutumia Mafundi Wataalamu kutoka ZECO na sio kutumia Mafundi wa Mitaani (Vishoka).
Afisa huyo amewataka Wananchi kuzima Vifaa vya Umeme mara baada ya kumaliza matumizi ili kujikinga na Madhara yanayoweza kujitokeza na kuleta athari kwa jamii.
Mapema akitoa Mafunzo ya Utumishi sahihi wa Majiko ya Gesi asilia Abdullah Hussein Hamad kutoka Kampuni ya Ismail LPG Campan amewataka Wananchi kutumia Nishati mbadala ya Majiko ya Gesi ya kupikia kwani yapo salama na hayana athari kwa jamii yakilinganisha na Nishati ya Kuni na Mkaa.
Sheha wa Shehia ya Mtumwajeni Rajab Ally Ngauchwa amewataka Wajumbe hao kushirikiana katika kuwahudumia Wananchi na kutoa taarifa za mapema wakati zinapojitokeza changamoto ndani ya Shehia zao.
Aidha ameishukuru Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar na Wafanyakazi wa Kampuni ya Majiko ya Gesi ya kupikia kwa kuwaelimisha matumizi bora ya Magesi hayo na kuahidi kuwa Mabalozi wazuri kwa wengine.