HeyBaadhi ya Wananchi waliohudhuria katika hafla ya Mkono kwa Mkono awamu ya Pili ambapo fursa mbalimbali zilitolewa na Changamoto kutatuliwa Kikwajuni Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Zanzibar.
Na Rahma Khamis, Maelezo
Waziri wa Uchumi na Buluu na Uvuvi, Mhe. Shaban Ali Othman, amesema Wizara inatarajia kutoa boti tatu za mitaa saba kwa vijana wa Mkoa wa Mjini Magharibi ili kupunguza msongamano wa vijana wasio na ajira.
Mhe. Othman ameyasema hayo katika Ukumbi wa Idriss Abdul-Wakil, Kikwajuni, wakati wa Kampeni ya Mkono kwa Mkono, ikiwa ni sehemu ya azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwasaidia vijana.
Aidha, Waziri huyo amefahamisha kuwa boti moja ya doria itatolewa kwa Kikosi cha Zimamoto (KZU) ili kurahisisha kazi zao na kuongeza ufanisi.
Akizindua kampeni ya Mkono kwa Mkono katika Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa, amesema Mkoa una mahitaji mengi kutokana na idadi ya wakazi wake ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo uvuvi, kilimo, ujasiriamali, na ufugaji.
Hivyo, amewataka vijana wa Mkoa huo kuchangamkia fursa zilizopo ili kujiinua kiuchumi na kuleta maendeleo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdalla Said, akizungumzia fursa zilizopo katika Wizara yake, amesema Wizara hiyo inaratibu na kutoa ufadhili wa masomo (scholarship) mbalimbali, ambapo nafasi 100 za ufadhili zimetolewa kutoka nchini Urusi.
Aidha, ameongeza kuwa Wizara pia inawaendeleza wazee ambao hawajui kusoma wala kuandika kwa kuwafundisha elimu ya watu wazima pamoja na kujenga vituo mbalimbali vya kujifunzia masomo ya Sayansi kwa vijana ikiwemo Jang’ombe.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Vuai Yahya Lada, amesema wamesajili miradi 471, ambapo miradi 156 imesajiliwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Aliwataka vijana kuzichangamkia fursa hizo ili kufikia malengo yao.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Fatma Muhammed Juma, amesema ZEEA imetoa Bilioni 31 kwa wajasiriamali kuwanufaisha wananchi, ambapo kwa Mkoa wa Mjini Magharibi wamepatiwa Bilioni 21 ili kujiendeleza na kukuza biashara zao.
Kampeni ya Mkono kwa Mkono ilizinduliwa rasmi katika Mkoa wa Kusini Unguja na kufungwa rasmi Novemba 27 katika Mkoa wa Mjini Magharibi.