Na Ashrack Miraji
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephaniel Sumaye, leo tarehe 27 ameongoza wananchi katika zoezi la kupiga kura la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo wanachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa, kitongoji na vijiji katika kituo cha Chake Chake, kilichopo wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
Akizungumza baada ya kupiga kura, Mhe. Sumaye aliwashukuru wananchi wa wilaya ya Lushoto kwa ukomavu wao wa kisiasa na kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo, akieleza kuwa ni ishara ya maendeleo katika demokrasia. Aliwataka wananchi kuendelea kushiriki kwa wingi ili kuchagua viongozi wanaowataka, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo linatakiwa kuwa la amani na utulivu.
“Tunashuhudia ukomavu mkubwa wa kisiasa kutoka kwa wananchi wa wilaya ya Lushoto. Kampeni zilifanyika kwa amani na hakuna malalamiko kutoka kwa vyama au wagombea,” alisema Mhe. Sumaye. “Ninawaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaowaongoza katika maendeleo ya jamii yetu.”
Mhe. Sumaye pia aliwasisitizia vyama vya siasa na wanachama wao kuheshimu kanuni za uchaguzi, akieleza kuwa malalamiko yoyote kuhusu uchaguzi yanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi.
Aidha, Mhe. Sumaye aliwataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima wakati wa uchaguzi, akiwataka waendelee na shughuli zao baada ya kupiga kura, ili kuepuka msongamano na usumbufu. na Alisisitiza kuwa hii ni siku ya mapumziko iliyotengwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili wananchi waweze kushiriki kwa wingi katika uchaguzi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Ikupa Mwaysoge, Msimamizi wa Uchaguzi wilaya ya Lushoto, alisema vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema asubuhi na hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza hadi sasa. Alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi na hali ni shwari katika maeneo yote ya uchaguzi.
“Tunawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi. Hii ni fursa muhimu ya kutimiza wajibu wa kikatiba, kuchagua viongozi bora watakaoweza kuleta maendeleo kwa jamii,” alisema Dkt. Mwaysoge.
Linoss Mwita, mkazi wa Lushoto, ambaye ni kijana, alisema kuwa aliona ni muhimu kushiriki katika uchaguzi huu, kwani ni haki yake ya kikatiba. Alisema kuwa ili kupata viongozi bora, ni lazima wananchi wawe na ushiriki mkubwa katika mchakato wa uchaguzi.
“Leo ni siku ya kupumzika, kama alivyosema Rais wetu, hivyo tunatumia siku hii kutekeleza wajibu wetu wa kikatiba. Napenda kuwahimiza vijana wengine kujitokeza kwa wingi ili kuchagua viongozi bora,” alisema Mwita.
Kauli mbiu ya uchaguzi wa mwaka huu ni: “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi.”