Benki ya NMB imekabidhi mabati 150 na madawati 150 kwa shule za msingi Kasanga, Kisasa, na Sawala zilizopo wilayani Mufindi, mkoani Iringa. Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 23 unalenga kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha sekta ya elimu na kurejesha kwa jamii, kwa mujibu wa sera ya benki hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Ndg. Benedicto Baragomwa, alisema benki hiyo imejikita katika kuhakikisha inawafikia wateja wake kote nchini kwa kusaidia maendeleo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu.
“Nilikutana na Mbunge wenu wa Mufindi Kusini, Mhe. David Kihenzile, ambaye alieleza changamoto ya madawati katika shule za Kasanga, Sawala, na Kisasa. Niliahidi kushughulikia changamoto hiyo, na leo, kupitia sera yetu ya kurejesha kwa jamii, tumefanikisha ahadi hiyo,” alisema Baragomwa.
Aidha, Baragomwa alizitaka kanda za Nyanda za Juu Kusini za benki hiyo kufanya tathmini ya hali ya shule na mahitaji mengine muhimu ili kusaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Aliongeza kuwa ombi la mabati 110 kwa ajili ya Shule ya Msingi Kasanga lipo kwenye mchakato wa kufanyiwa kazi ili kupunguza mzigo wa michango kwa wazazi na walezi.
Shukrani za Mbunge na Walimu
Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, aliishukuru NMB kwa msaada huo, akisema umeondoa changamoto ya wanafunzi kuketi chini na mvua kuvuja madarasani.
“Msaada huu si tu unasaidia kuboresha mazingira ya wanafunzi, bali pia unawaondolea wazazi mzigo mkubwa wa michango. Ni wakati sasa kwa wananchi kutumia benki ya NMB kwa kufungua akaunti na kujiwekea akiba, sambamba na kunufaika na mikopo ya papo hapo kupitia simu za mkononi,” alisema Kihenzile.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kasanga, kwa niaba ya shule zingine zilizopokea msaada huo, alisema changamoto ya wanafunzi watano kushirikiana dawati moja badala ya watatu sasa imepata suluhisho.
Maoni ya Wazazi na Walezi
Baadhi ya wazazi na walezi walipongeza benki ya NMB kwa msaada huo, wakiahidi kuwa mabalozi wa benki hiyo kwa kuhamasisha wananchi kuitumia ili kuendelea kunufaika na huduma zake na msaada zaidi kwa jamii.
Msaada huu ni moja ya hatua muhimu za kuimarisha elimu wilayani Mufindi, huku NMB ikiendelea kuonyesha dhamira yake ya kuleta maendeleo katika jamii kwa vitendo.