Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Katiba na sheria Profesa Palamagamba Kabudi ametoa rai kwa wananchi nchini kujitokeza kupinga ukatili wakijinsia ili kutokomeza tatizo hilo nchini na kuwa na nchi yenye usawa katika masuala mbalimbali.
Wito huo ameutoa leo Novemba 25,2024 jijini Dar es salaam wakati Akizindua rasmi siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia wenye kauli mbiu ya kuelekea miaka 30 ya Beijing changua kutokomeza Ukatili wa kijinsia.Amesema ukatili wakijinsia unapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
Ameongeza kuwa suala la ukatili wa kijinsia ni suala la aibu linalobeza kundi kubwa katika jamii na si la kifahari kulitetea.
”Suala hilo la ukatili wa kijinsia ni suala baya na linalohitaji kutokomezwa na hali budi kuchukuliwa hatua stahiki.
”Katika sheria zetu mbalimbali tunasheria nyingi zinazopinga ukatili wa kijinsia na zinaelezea masuala hayo na kutoa adhabu kali ikiwemo sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 mkiisoma sheria hiyo imeelezea ukatili katika maeneo mengi,”amesema na kuongeza
”Miongoni mwa sheria hiyo imeeleza ukatili wa kutowanunulia nguo watoto wao,kutonunua Chakula kwa watoto ni kosa la jinai na lipo ndani ya adhabu,usipowatunza watoto lakini pia sheria ya huduma ya msaada wa sheria sura ya 21 nayo inazungumza utoaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto.
Ameongeza kuwa licha ya Tanzania kupiga hatua katika mapambano hayo bado inahitaji kupiga hatua zaidi na kutaka kila mmoja awe balozi wa kupinga ukatili wa kijinsia.
Prof. Kabudi amesema ni adhima ya taifa kuungana katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo vinagharimu maisha ya watu wengi.
”Sasa ni wakati wa kila mmoja wetu kuwa balozi wa kuhakikisha anapinga ukatili wa kijinsia kwani kunasheria mbalimbali zinatambua masuala hayo ya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dk. Monica Muhoja amesema kuna haja ya kuongeza kasi zaidi katika kumuinua mwanamke sambamba na kutungwa kwa sheria maalum za kupinga ukatili wa kijinsia.
Amesema wanawake na watoto wameendelea kuwa waathirika wa vitendo hivyo na kwamba wako tayari kubainisha mapungufu yaliyopo kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa kuwa walifanya utafiti.
“Mwaka huu tumekuja na maombi mengine ambapo tunaomba Serikali kuweza kuyashughulia ikiwemo ombi la
kutumia juhudi za kuwafikishia kwenye agenda za kiusalama kwa kuhakikisha kuwa masuala ya ukatili wa kijinsia yanaingizwa rasmi katika mipango na mikakati ya kiusalama ya kitaifa lakini pia serikali kuomba kutungwa kwa sheria mahsusi ambayo italinda jamii hasa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia”,Amesema.
Naye Mkurugenzi wa WiLDAF (Women in Law and Development in Africa),Anna Kulaya amesema dhamira ya Kampeni hiyo ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia huku ikikuza usawa,heshima na haki kwa wote.
“Leo ni siku muhimu sana kwetu sote tunapoanza safari ya kuelekea Siku 16 za Uanaharakati wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Hii ni fursa ya kipekee ya kushirikiana, kuhamasisha, na kuchukua hatua za pamoja dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia kwa ajili ya jamii yenye usawa, heshima, na haki kwa wote.