*Afunga kwa kishindo Kampeni za CCM Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mbinga
*Asema CCM ni tumaini la Watanzania; Ipate kura za Ndiyo
*Akumbusha kuwa miradi ya maendeleo iliyopo ni kielelezo cha viongozi makini wa CCM
Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 27 Novemba 2024 kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa pia ni utekelezaji wa haki ya kikatiba.
Kauli hiyo ameitoa Novemba 26, 2024 wakati wakihitimisha kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Vijijini.
Akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika shughuli hiyo ya ufungaji wa kampeni, Kapinga amewaasa wajitokeze kwa wingi kuchagua wagombea kutoka CCM kwani ndio wenye uchungu na maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii.
“Chama cha Mapinduzi (CCM) ni tumaini la watanzania wanaohitaji maendeleo, hivyo ifikapo Novemba 27, 2024 jitokezeni katika vituo vya kupigia kura ili mkachague Viongozi kutoka CCM watakaosimamia miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika Mitaa na Vijiji.” Amesema Kapinga
Ameeleza kuwa, CCM imekuwa na utaratibu mzuri wa kuwasimamia Viongozi wake ili kuhakikisha wanafikisha maendeleo kwa wananchi kama Ilani ya CCM inavyoelekeza.
Mhe. Kapinga ameweka mkazo kuwa, miradi ya maendeleo inayopelekea upatikanaji wa huduma za Umeme, Maji, Elimu, Afya, Kilimo na Barabara ni matokeo mazuri ya Viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya vitongoji hadi Taifa.