Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Rehema Lyana, imemhukumu Bw. Michael Henry Msangawale, aliyekuwa Afisa TEHAMA wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji Kampasi ya Dar es Salaam, kwa kosa la kudai rushwa ya ngono. Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mshtakiwa kukiri kosa kupitia makubaliano ya maridhiano (plea-bargaining) katika Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 16/2022.
Bw. Msangawale alishtakiwa kwa kosa la kudai rushwa ya ngono, kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (marejeo ya mwaka 2019), pamoja na Jedwali la 21 la Aya ya Kwanza ya Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi (EOCCA).
Kwa mujibu wa mashtaka, mshtakiwa alikataa kumwekea matokeo katika mfumo mwanafunzi mmoja, akimtaka kutoa rushwa ya ngono ili aweze kuendelea na masomo yake katika ngazi ya Diploma.
Wiki iliyopita, Bw. Msangawale aliomba kufanya makubaliano ya maridhiano na Mahakama ilikubaliana na ombi hilo. Alikiri kosa na kuhukumiwa kulipa fidia ya shilingi milioni kumi, ambazo zitatolewa kwa mwanafunzi aliyelazimishwa kutoa rushwa hiyo ya ngono.
Hukumu hii ni mfano wa hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya vitendo vya rushwa ya ngono, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na rushwa katika sekta ya elimu nchini.