Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini na Kaskazini Chiza Marando akikanusha kuenguliwa kwa mawakala wa chama ACT-Wazalendo wataoshuhudia uchaguzi wa Serikali za mitaa kesho.
……
Na Mwandishi MaalumT, unduru
MSIMAMIZI wa uchaguzi wa Serikali za mitaa katika jimbo la Tunduru Kusini na Kaskazini mkoani Ruvuma Chiza Marando,amekanusha kutengua uteuzi wa majina ya mawakala wa Chama cha ACT-Wazalendo wataoshuhudia zoezi la kupiga na kuhesabu kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika kesho.
Amesema,kilichofanyika ni kuwaondoa wagombea waliopitishwa na Chama hicho kuwa mawakala kwenye vituo vya kupigia kura na badala yake wanatakiwa kubaki wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
“Leo asubuhi nilipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wasimamizi ngazi ya kata kwamba Chama cha ACT kimeleta majina ya mawakala ambao ni wagombea katika uchaguzi huo,nilichokifanya nimewaita viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wakiongozwa na Mtutura Abdala Mtutura kuwaambia kwamba walichokifanya siyo sahihi”alisema Marando.
“Sheria ya Uchaguzi inakataza mgombea kuwa wakala wa chama cha Siasa,wakakubali kwenda kutafuta mawakala wengine,sasa nashangaa kuona taarifa iliyoandikwa kupitia mitaa ya kijamii kwamba Tunduru tumetengua majina ya mawakala wa Chama hicho”alisema.
Aidha alitaja watu wanaopaswa kushuhudia uchaguzi huo ni mawakala walioteuliwa na vyama vyenye wagombea na siyo wagombea,wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,Jeshi la Polisi,na watu wengine wanaotambulika kisheria.
“kuna madhara makubwa ya kutumia wagombea kuwa mawakala,kunaweza kutokea uvunjifu wa amani na pia kutoa nafasi kwa wagombea kuendelea kufanya kampeni siku ya kupiga kura wakati siyo siku ya kufanya kampeni,tuwaache mawakala walioteuliwa na vyama vyao waendelee kushuhudia zoezi zima la upigaji kura na kuhesabu”alisema.
Alisema,uchaguzi huo utafanyika kwa amani na utulivu na mgombea atakayeshinda atatangazwa mshindi bila upendeleo wowote ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye kupiga kura kwa kuwachagua viongozi wanaowataka.