……….
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa tahadhari hiyo,leo kuwa lipo tayari kudhibiti vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na kuchukua hatua kali dhidi ya watu au vikundi vitakavyojaribu kuvuruga uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano na wadau wa uchaguzi uliofanyika katika Uwanja wa Polisi Mabatini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbrod Mutafungwa, amesema jukumu la polisi ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usalama na kwamba kila mwananchi awe na uhuru wa kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura bila kuhofia vitisho vya aina yoyote.
Mutafungwa amesisitiza kuwa mikutano ya kampeni inapaswa kufanyika kwa utulivu, polisi watahakikisha usalama wa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi akiwemo viongozi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Amewaonya wanasiasa na wafuasi wao kuepuka vitendo vya kuwatisha wananchi au kuzuia haki yao ya kupiga kura, watakaokiuka watakumbana na mkono wa sheria.
“Polisi tunalo jukumu la ulinzi na usalama kuhakikisha unazingatiwa ili kuwe na utulivu, usalama na amani.Sote tuone umuhimu wa kufanya uchaguzi kwa amani, ili watu wapate nafasi ya kutimiza wajibu wao na haki yao ya kikatiba. Hatuwezi kuvumilia vitendo vya kuvuruga uchaguzi na kuathiri amani,”amesema.
Aidha, Mutafungwa ameonya mikusanyiko isiyo halali kuwa itadhibitiwa na wananchi wanapaswa kuepuka kujiingiza katika vikundi vyovyote vinavyohamasisha vurugu huku akiwahimiza viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani katika makanisa na misikiti ili kuhamasisha wananchi kutimiza wajibu wao kwa amani.
Kamanda huyo wa pia ameitaka jamii na wadau wa uchaguzi kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa usalama kwani usalama wa wananchi utahakikisha uchaguzi wa mwaka 2024 unakuwa na matokeo bora na ya amani.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Jamal Babu, amesema kuwa CCM iitahakikisha wafuasi wake wanazingatia sheria za uchaguzi na kusisitiza kulinda amani kuwa uchaguzi unapaswa kuwa salama kwa manufaa ya maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu (CHAWATA) Wilaya ya Kwimba, Julius Musa, ameeleza kuwa walemavu wanahitaji mazingira salama na amani ili kutekeleza haki zao za kupiga kura, kwani hawana pa kwenda ikiwa vurugu zitajitokeza.
Amesema kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi, bila kujali hali yake kwa kuzingatia katiba , kuwa na uhuru wa kushiriki uchaguzi kwa amani na bila kutishiwa.