Na Sophia Kingimali
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi Novemba 27, 2024, kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. Amewahakikishia wananchi kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa amani na utulivu, huku Jeshi la Polisi likiwa limejipanga vizuri kuhakikisha usalama unadumishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 25, 2024, Chalamila alisema hali ya usalama katika mkoa wa Dar es Salaam iko shwari, na yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Niwatoe wasiwasi wananchi. Jitokezeni mkapige kura, na mkimaliza rudini kwenye shughuli zenu. Askari wetu wako kila kona, tena kwa wingi, kuhakikisha amani inapatikana,” alisema.
Mkuu wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo zimekuwa nguzo ya ustahimilivu wa kitaifa. Alisema ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi huu utachochea maendeleo ya demokrasia nchini.
“Uchaguzi huu si tu kipimo cha demokrasia, bali unapaswa kuwa huru na haki, unaoakisi zile 4R ambazo Rais Dkt. Samia ameziasisi. Ni fursa ya wananchi kuchagua viongozi wanaowaamini,” aliongeza.
Chalamila alisema Dar es Salaam ina jumla ya mitaa 564, na wanatarajia kuchagua wenyeviti 564 pamoja na wajumbe mbalimbali. Aidha, alieleza kuwa vyama vingi vimeshiriki katika mchakato wa uchaguzi, hivyo kila chama kina nafasi ya kuwa na wawakilishi wake.
“Licha ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea waliondolewa kwenye mchakato, vyama vingi vimesimamisha wagombea katika maeneo mengi. Tunawataka wapenzi wa vyama hivi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi,” alisema.
Kuhusu janga la kuporomoka kwa jengo la ghorofa tatu katika eneo la Kariakoo, Chalamila alisema zoezi la uokoaji bado linaendelea. Alibainisha kuwa Waziri Mkuu atatoa taarifa rasmi hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na maelezo kuhusu lini wafanyabiashara wa eneo hilo wataweza kufungua biashara zao.
“Pia, tutatoa taarifa za hatua zilizofikiwa, ikiwemo ubomoaji wa jengo hili, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa eneo hilo,” alisema Chalamila.
Wananchi wa Dar es Salaam wanatarajiwa kushiriki kwa wingi kwenye zoezi hili muhimu la kidemokrasia, huku mamlaka zikiahidi kuhakikisha amani na usalama vimetangulizwa.