Na. Mwandishi Jeshi Polisi Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawatafuta watuhumiwa waliohusika katika tukio la kumshambulia na kumjeruhi mtoto wa kike (16) (jina limehifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Nadaale, wilaya ya Longido Mkoani Arusha.
Akitoa taarifa hiyo leo Novemba 25, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kitumbeine iliyopo wilayani Longido lakini aliachishwa masomo na kuozeshwa kwa mwanaume aitwaye Mungere Arkaswai mkazi wa kata ya Engaruka Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limekemea vikali tabia ya baadhi ya watu wanaofanya vitendo vya ukatili na unyanyasaji ikiwemo wanaoozesha watoto kuwa litawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Sambamba na hilo, limetoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana na Polisi kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii kuacha vitendo hivyo.